Ssaru akana madai ya kuwa katika mahusiano na Trio Mio

Muhtasari

• Mwanamuziki wa mtindo wa kufoka Sylivia Ssaru amekana madai yaliyozagaa mitandaoni siku za hivi karibuni kwamba ako katika mahusiano ya kimapenzi na msanii mchanga Trio Mio

• Picha za wawili hao zilizozua gumzo mitandaoni zilionekana baada ya Ssaru na Trio Mio kuzindua kibao chao kipya kabisa kwa jina ‘Kichwa Tu’

Sylivia Ssaru
Image: Facebook

Mwanamuziki wa mtindo wa kufoka Sylivia Ssaru amekana madai yaliyozagaa mitandaoni siku za hivi karibuni kwamba ako katika mahusiano ya kimapenzi na msanii mchanga Trio Mio

Madai hayo yalisambazwa mitandaoni baada ya picha za wawili hao wakiwa Pamoja katika mkao fulani unaodokeza huba kati yao kuzagaa sana.

Picha za wawili hao zilizozua gumzo mitandaoni zilionekana baada ya Ssaru na Trio Mio kuzindua kibao chao kipya kabisa kwa jina ‘Kichwa Tu’ ambapo pia walimshirikisha msanii mwenye ujuzi wa shughuli hizi, Timmy Tdat.

Hiki ni kibao cha pili ambacho msanii Ssaru wanafanya na kijana Trio Mio baada ya kile cha kwanza cha ‘Sipangwingwi’ walichoshirikishwa na msanii Exray kupata ufanisi mkubwa mpaka kupelekea wasanii hao kupata mialiko ya kutumbuiza katika hafla mbali mbali za kisiasa.

Trio Mio
Image: Instagram

Ssaru akizungumza katika mahojiano na runinga ya TV47 wikendi iliyopita, amekana madai ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na kijana huyo mdogo na kusema kwamba wale wanaosema ana mahusiano na Trio Mio ni kama kumuonea tu kijana wa watu ambaye hajui hata mapenzi ni nini.

“Jamani hapo hata kijana mwenyewe mnamuonea bure, mwacheni asome jamani,” alisema Ssaru.

Itakumbukwa hii si mara ya kwanza kwa msanii Ssaru kukumbwa na madai ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na kijana Trio Mio.

Katika ukurasa wake wa Instagram wakati akifanya Q&A na mashabiki wake, shabiki mmoja aliwahi muuliza swali hilo pia ila Ssaru alikana madai hayo na kusema kwamba Trio Mio ni kama ndugu yake mdogo na hawezi kuwa katika mahusiano ya kimapenzi na yeye na kwamba kinachowaweka Pamoja ni kazi za kimuziki tu.