Burale aelezea jinsi alijiungwa klabu ya wacheza uchi

Muhtasari

• Robert Burale ameelezea jinsi alijipata kwenye klabu ya wacheza uchi nchini Uingereza akiwa masomoni kabla ya kupata wokovu

• Alipigana vita vya kujitoa katika mazoea ya kuenda kwenye sehemu za burudani za wacheza uchi kwa muda wa miaka saba

Robert Burale
Image: Facebook

Mzungumzaji wa motisha na mhubiri Robert Burale ameelezea jinsi alivyoshawishiwa na Rafiki zake na kujiunga na klabu ya watu wanaocheza bila nguo, almaarufu ‘strippers club’

Akizungumza na mchekeshaji Oga Obinna, Burale amesema alishawishiwa na rafiki zake waliokuwa wakisoma naye nchini Uingereza na mwisho wa siku akajipata katika klabu hiyo na kushindwa kujitoa kwa miaka saba.

“Nilishawishiwa na rafiki zangu tukaingia huko. Nilipoingia kule nilijiambia kwamba naenda kujionea tu kwa mara moja na niachane kabisa lakini niliteseka kuacha kuenda kule kwa miaka saba,” alisema Burale.

Alipokuwa akisoma katika chuo cha Leicester nchini uingereza, Burale alisema kipindi hicho hakuwa amepokea wokovu na alichokiona katika klabu ya wacheza uchi mara ya kwanza kilimnata kichwani na akashindwa kujinasua katika vita vyake na nafsi yake vilivyodumu muda wa miaka saba.

“Wacheza uchi hao wanacheza densi na wewe wakiwa wamekuangalia moja kwa moja machoni pako na hapo unajihisi kama mfalme, na hapo lazima tu utumie pesa nyingi ili kuendelea kupata raha,” Burale alieleza.

Mchungaji huyo ameelezea jinsi mazoea ya kuenda katika klabu hiyo yalimfyonza na kumkausha mifuko yake kwa sababu pesa zake nyingi alikuwa akizitumia pale.

“Siwezi hata mara moja kumshauri kijana mdogo ambaye anasema kwamba anataka kujaribu kuingia pale, siwezi,” alisema Burale

Mhubiri Burale amesema kwamba ilimchukua muda wa miaka saba kupigana vita na nafsi yake kujitoa katika mazoea ya kuenda pale na miaka mingine mitatu ya kujikwamua kabisa na baadae kupokea wokovu.