"Tumsamehe tu, hakujua maana ya Confederate flag" Diamond atetewa kuhusu madai ya ubaguzi wa rangi

Muhtasari

•Wanamitandao wameendelea kutoa hisia tofauti kuhusiana na suala hilo huku wengi wakimshtumu Diamond kwa ubaguzi wa rangi.

•Kimambi amesema ana uhakika kuwa iwapo Diamond angejua maana ya bendera hiyo asingekubali itumike kwenye video yake

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Nyota wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu kama Diamond Platnumz ameendelea kukosolewa mitandaoni kufuatia matumizi ya bendera ya Shirikisho (Confederate Flag)  kwenye  video ya wimbo wake mpya 'Gidi'.

Shirikisho lilikuwa ni kundi la majimbo ya kusini ambayo yalipigana kudumisha utumwa wakati wa Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Marekani - na bendera hizo zinaonekana kama ishara ya mivutano ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani.

Wanamitandao wameendelea kutoa hisia tofauti kuhusiana na suala hilo huku wengi wakimshtumu kwa ubaguzi wa rangi huku wengine wakijitokeza kumtetea mwanamuziki huyo tajika.

Mwanaharakati mashuhuri nchini Tanzania Mange Kimambi ni mmoja wa waliojitokeza kumtetea Diamond. Kulingana na Kimambi, Diamond hakufahamu maana ya bendera hiyo aliporuhusu  itumike kwenye video na kwa hilo amewasihi Watanzania washushe roho zao na wakubali kumsamehe.

"Naona wengi mmetaka ni -address hili swala la confederate flag kwenye video mpya ya Diamond, mi naona tumsamehe tu. Mi nimemuonea huruma tu maana nimeona ni kwamba tu hakujua maana ya hiyo confederate flag. Labda tu kama mtu alisoma historia ya utumwa haswa kwa upande wa marekani au ana exposure sidhani kama anaweza kujua hii bendera ina maana gani. Kwa hakika hata wanaomzunguka hawana exposure vile vile kwa hiyo hakuna aliejua maana ya hiyo bendera." Kimambi amesema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Diamond Platnumz
Image: BBC

Mwanaharakati huyo amesema ana uhakika kuwa iwapo Diamond angejua maana ya bendera hiyo asingekubali itumike kwenye video yake.

Kimambi hata hivyo amemshauri staa huyo wa Bongo kujiandaa kwa maswali magumu ambayo huenda yakafuata kuhusiana na suala la bendera hiyo

"Kuna siku lazma atajikuta anaulizwa kuhusu hili akiwa nchi za nje hususan marekani. Maana marekani hawana mchezo kabisa kwenye swala la hii bendera. Kwa hivyo cha kufanya ni ajipange tu siku akiulizwa atajibu nini, maana kama kuna siku atafanya mahojiano marekani piga ua hili suala  lazma watamkalia nalo kooni mpaka aombe msamaha . Hawatomwelewa mpaka aombe msamaha. Wamarekani weusi wako na hisia kubwa kuhusu suala la hii bendera" Alisema Kimambi.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Kimambi na aliyekuwa mpenzi wa Diamond Zari Hassan kutofautiana na kutupiana vijembe mitandaoni.

Hivi majuzi wawili hao walizozana kuhusu masuala mbalimbali na kutupiana maneno makali hadharani kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.