'Alinibadilisha kutoka kuwa jike dume,' Dadake Diamond amsifia mumewe licha ya changamoto za ndoa yake

Muhtasari

•Darleen hata hivyo aliweka wazi kuwa angali anampenda mume wake na huwa wanawasiliana mara kwa mara.

•Darleen alisema mumewe amejengea heshima kubwa maishani huku akikiri kwamba huwa anahuzunika kila anaposikia watu wakimdhihaki mfanyibiashara huyo. 

Queen Darleen na mumewe Isihaka
Queen Darleen na mumewe Isihaka
Image: HISANI

Mwanamuziki Mwanajuma Abdul Juma almaarufu Queen Darleen amefunguka kuhusu ndoa yake na mfanyibiashara Isihaka Mtoro.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Darleen ambaye ni dada mkubwa wa Diamond Platnumz alikiri kuwa hana uhakika iwapo bado yuko kwenye ndoa ama tayari alishatemwa.

Darleen hata hivyo aliweka wazi kuwa angali anampenda mume wake na huwa wanawasiliana mara kwa mara.

"Kiukweli mpaka sasa sijijui. Sijui kama niko kwenye ndoa ama siko kwenye ndoa. Nampenda sana mume wangu. Popote alipo ajue kwamba nampenda sana sana. Yeye ndiye anajua kama niko naye ama siko naye," Darleen alisema.

Mwanamuziki huyo alisema licha ya changamoto zote zilizokumba ndoa yake hapo awali angali anathamini Bw. Mtoro kwa kuwa alicheza nafasi kubwa katika kubadilisha maisha yake.

Darleen alisema mumewe amejengea heshima kubwa maishani huku akikiri kwamba huwa anahuzunika kila anaposikia watu wakimdhihaki mfanyibiashara huyo. 

"Siwezi kuelezea jinsi ninavyompenda mume wangu. Ni mwanamume ambaye alikuja kunibadilisha kwenye maisha yangu ya kuwa jike dume kama walivyokuwa wakiniita na kuja kuwa mke mpaka kuwa mzazi aliyezaa kwenye ndoa. Nina mtoto wa kwanza ila wengi hawakufahamu. Ameniheshimisha sana. Ninaposikia mtu akimdhihaki kwa maneno mabaya najiskia vibaya sana. Mtu akimsema, naumia. Hapo ndipo ninapogundua kuwa bado nina mapenzi naye," Darleen alisema.

Mnamo mwaka jana uvumi ulitanda kuwa mwanamuziki huyo ametemwa na mumewe baada ya kuwa katika ndoa kwa kipindi kifupi.

Haya yalijiri baada yake kuacha kupakia picha za mfanyibiashara huyo kwenye kurasa zake za kijamii kama ilivyokuwa ada yake.