Eric Omondi kutembelea vituo vya habari kupigia debe 'Play75%Local'

Muhtasari

• Eric Omondi kuanza kutembelea vituo vyote vya habari ili kufanikisha mchakato wa muziki wa Kenya kuchezwa kwa asilimia 75.

Erick Omondi nje ya majengo ya bunge
Erick Omondi nje ya majengo ya bunge
Image: JULIUS OTIENO

Kama ulikuwa unafikiria kwamba mchekeshaji Eric Omondi alikuwa anafanya ucheshi wake kama wengi walivyomzoea katika kampeni zake za kuagiza vyombo vyote vya habari nchini Kenya kucheza asilimia 75 ya muziki wa Kenya basi ulikosea.

Mchekeshaji huyo anaendelea kupiga hatua kubwa katika mchakato wake wa kupigia debe azma hilo la kuhakikisha muziki wa Kenya unapata nafasi ya kuchezwa kwenye stesheni zote kwa asilimia 75.

Huku taifa lingisubiri mswada wake huo aliowakabidhi wabunge waujadili na kuupitisha ili kusainiwa kuwa sheria, Omondi ametangaza kuanzisha kampeni za kutembelea kila kituo cha habari nchini ili kutoa pendekezo lake la kutaka muziki wa Kenya kuchezwa kwa asilimia 75 ya miziki yote.

Akiandika kwenye Instagram yake, Omondi alisema kwamba atakuwa anatembelea vituo vyote na kusema tayari ashaanza na kituo cha KBC ambapo alidokeza kwamba mazungumzo yake na mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo la serikali alikubali kwamba wameanza mazungumzo na washikadau katika shirika hilo ili kutekeleza amri ya kucheza miziki ya Kenya kwa asilimia 75.

“Leo nilitembelea mkurugenzi mtendaji waw a KBC, Dkt Naim Bilal katika ofisi yake ili kuzungumzia suala la kuchezwa kwa miziki ya Kenya kwa asilimia 75. Nitakuwa natembelea vituo vyote vya habari lakini niliona ni vizuri nianze na shirika hili la kitaifa kwa sababu mawimbi ya mitabendi zao hufika katika kila eneo la taifa hili na wako na vituo vingi vya habari chini ya mwavuli wao. Tulikubaliana kufanya kazi Pamoja kuhakikisha azma hili linatimia hivi karibuni Zaidi,” aliandika Omondi.

Hili linakuja siku moja tu baada ya taarifa ya mchekeshaji huyo kutaka muziki wqa Kenya kwa asilimia 75 kuchapishwqa kwenye gazeti moja mchini Uholanzi.

Wiki mbili zilizopita Omondi alizua kioja baada ya kusema kwamba alikuwa radhi kukita kambi katika majengo ya bunge la kitaifa mpaka mswada huo ujadiliwe na kuamuriwa lakini baadae akaondoka baada ya kusema kwamba wabunge walimsihi kufanya hivo kwa hakikisho kwamba wataangazia mapendekezo ya mswada wake.