Eric Omondi aapa kukita kambi bungeni, kususia chakula hadi mswada aliowasilisha upitishwe

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo alijifungia kwenye sanduku la vioo na kubebwa juu juu hadi nje ya bunge ambako ameapa kukaa hadi wakati mswada wake wa kupigania muziki wa Kenya kuchezwa zaidi utakapopitishwa.

Erick Omondi nje ya majengo ya bunge
Erick Omondi nje ya majengo ya bunge
Image: JULIUS OTIENO

Mchekeshaji mashuhuri Eric Omondi ameamua kupeleka kampeni zake za kupigania muziki wa Kenya katika kiwango cha juu zaidi.

Siku ya Jumatano mchekeshaji huyo alijifungia kwenye sanduku la vioo na kubebwa juu juu hadi nje ya bunge ambako ameapa kukaa hadi wakati mswada wake wa kupigania muziki wa Kenya kuchezwa zaidi utakapopitishwa.

Omondi ambaye alikuwa amekalia kiti kilichokuwa ndani ya sanduku kubwa la vioo lenye maandishi 'Play 75% Kenyan' alibebwa na wanaume watano na kuwekwa kwenye lango la bunge na kuonekana kustarehe pale.

Nimeingia kwenye majengo ya bunge na nitakaa hapa kwa wakati ambao itachukua muswada wa muziki wa Kenya kuchezwa 75% utakapopitishwa" Eric aliandika chini ya video ambayo alipakia kwenye mtandao wa Instagram.

Mchekeshaji huyo aliendelea kuapa kuwa hatakula chochote katika kipindi chote ambacho atasalia pale nje ya bunge.

Alisema kwamba  hatabanduka pale bila kujali muda ambao itachukua muswada wake kupitishwa huku akidai kwamba hata yuko tayari kufa njaa. 

"Natangaza rasmi mgomo wa njaa, ikibidi nikae hapa kwa miezi miwili na iwe hivyo. Nikifa hapa kutokana na njaa na iwe hivyo!!!!" Omondi alisema.

Mwaka jana Eric Omondi aliwakabidhi wabunge Babu Owino na Jaguar mswada unaopendekeza muziki wa wasanii wa hapa nchini uchezwe zaidi katika vituo na maeneo ya burudani.