"Waite GSU!" Eric Omondi aapa kusimamisha shoo ya Konshens mkesha wa mwaka mpya

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo amesema juhudi zake zote za kupigania muziki wa Kenya zitakuwa zimeangulia patupu iwapo hafla hiyo itaruhusiwa kufanyika.

•Omondi amelalamika kwamba waandalizi wa hafla hiyo wanapanga kukaidi makubaliano yao ya kuachia bendi ya Sauti Sol kufunga hafla hiyo.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji mashuhuri aliyezingirwa na sarakasi si haba katika taaluma yake Eric Omondi ameapa kufanya kila awezalo kusimamisha shoo ya nyota wa Dancehall  Garfield Spence almaarufu kama Konshens ambayo imepangwa kufanyika Ijumaa usiku.

Alipokuwa anahutubia wanahabari siku ya Jumatano, Omondi aliapa kutoruhusu mwanamuziki huyo kutoka Jamaica kuwa kivutio kikuu katika hafla ambayo itafanyika Carnivore mkesha wa mwaka mpya.

Mchekeshaji huyo amesema juhudi zake zote za kupigania muziki wa Kenya zitakuwa zimeangulia patupu iwapo hafla hiyo itaruhusiwa kufanyika.

"Naahidi Wakenya, haiwezekani Konshens akawa kivutio kikuu na kutumbuiza wa mwisho katika hafla hii. Hafla hiyo haitafanyika. Waite polisi wote, waite GSU, haiwezi fanyika. Hii ni kwa sababu tukiruhusu ifanyike , vita vyetu vitakuwa vimeangulia patupu. Haitafanyika, nitafanya kila niwezalo, watanitoa kwa jukwaa hilo" Omondi alisema.

Alisema iwapo hafla hiyo itaruhusiwa kufanyika basi atakuwa amepoteza wakati wake na fedha nyingi  alizowekeza huku akilalamika kwamba hajakuwa akifanya kazi yake ya ucheshi tangu mwezi Oktoba akishughulika na kupigania muziki wa Kenya.

Omondi amelalamika kwamba waandalizi  wa hafla hiyo wanapanga kukaidi makubaliano yao ya kuachia bendi ya Sauti Sol kufunga hafla hiyo.

"Tulijadiliana na kukubaliana kwamba kutakuwa na msanii wa Kenya, haswa Sauti Sol ambao watatumbuiza wa mwisho. Mimi sio mjinga, naweza hisi mambo yakibadilika, kuna simu hazichukuliwi. Kuna wenye wanasema ati jambo hilo halijalishi. Kwa sasa muziki wa Kenya unainuka" Omondi alisema.

Konshens aliwasili nchini siku ya Jumanne na kupokea makaribisho ya kufana katika uwanja wa ndege wa JKIA. Anatarajiwa kutumbuiza mkesha wa mwaka mpya wa 2022.