Eric Omondi awapasha wasanii wanaosema amefeli

Muhtasari

• Eric akizungumza kwa ghadhabu kwenye video ambayo aliweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, Februari 11,  amesema kwamba wasanii wa humu nchini Pamoja na baadhi ya wachekeshaji ni wazembe

• Katika video hiyo, Omondi amewauliza wabaya wake maswali mengi ambayo pengine yatahitaji mwaka mzima kujibiwa.

Eric Omondi
Image: Instagram

Mchekeshaji mwenye utata ameamua kuvunja kimya na kutema yaliyoko moyoni mwake, safari hii bomu lake likiwalenga wasanii nchini Kenya wanaomchimba mikwara kwamba amepoteza vita vyake vya kutaka muziki wa nchini upewe asilimia 75 katika sehemu za burudani na vituo vya habari.

Eric akizungumza kwa ghadhabu kwenye video ambayo aliweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, Februari 11,  amesema kwamba wasanii wa humu nchini Pamoja na baadhi ya wachekeshaji wanasema kwamba amepoteza mwelekeo katika kazi zake na sasa anaanza kuchafua Sanaa ya muziki.

Katika video hiyo, Omondi amewauliza wabaya wake maswali mengi ambayo pengine yatahitaji mwaka mzima kujibiwa.

“Maneno mitaani ni kwamba Eric Omondi amepoteza, na hili linakuja kutoka kwa wasanii, waimbaji na hata aibu Zaidi baadhi ya wachekeshaji. Kama nimepoteza vile mnasema, inakuaje mimi ndio huyu niko katika anga tua nikielekea Juba, Sudan Kusini kwa tamasha la mtu mmoja? Kama nimepoteza, inakuaje hii wikendi niko na show tisa na nyinyi hamna hata moja na mko tu mmekaa nyumbani hamna hata moja? Tumia vichwa vyenu vizuri. Nimeghairisha shughuli zangu za kibiashara ili kutetea na kuwapigania lakini hamuoni. Mpaka nimeingia katika mizozo na baadhi ya wafadhili wangu hadi wengine wananipeleka mahakamani kwa sababu yenu. Amkeni, simama na fikirieni,” Omondi alifoka

Mcheshi huyo ameenda mbele kuorodhesha baadhi ya show ambazo anatarajiwa kufanya wikendi hii katika nchi mbili tofauti ikiwemo Tanzania na Sudan Kusini na kuwataka wasanii wamheshimu kwa kile anachojaribu kuwapigania.

Amewakashfu wasanii wa humu nchini na kusema wao ni wazembe na pia wachekeshaji wa humu nchini ni wa kuchosha na hawajui kazi yao ya ucheshi.

Amewapasha kwa kuwaambia kwamba yeye mwenyewe ni gumzo la kitaifa kwa sababu ameenda mpaka kawenye majengo ya bunge kuwapigania hali ya kuwa wao wametebwereka tu.

Amesema kwamba wasanii nchini hawana pesa kwa sababu ya uzembe wao. Amewaambia kwamba mwaka huu nchi inapojiandaa kuwatuma nyumbani wanasiasa ambao hawajafanya kazi kwa wananchi na yeye atahakikisha wasanii wazembe wameoneshwa mlango nje ya Sanaa ya Kenya.