Weezdom: Wasanii wa injili walinitenga, nina watoto wengi

Muhtasari

• Weezdom amefunguka sababu ya kujitoa katika muziki wa injili na kuingia mitindo ya kidunia ni kwamba alitengwa na jamii ya wainjilisti kwa kuwa na watoto wengi nje ya ndoa.

Weezdom
Image: Maktaba

Weezdoma anaendelea kupiga mishe kutembelea vituo vya habari mbalimbali nchini kwa kutangaza ujio wake kimuziki baada ya kimya cha muda mrefu, safari hii akirudi na ngoma za isiyo ya injili na ambayo amemshirikisha mwanasosholaiti Manzi wa TRM ambaye pia amekiri mara kadhaa tu kwamba ndiye mpenzi wake mpya baada ya kuachana na Mylee Staicey.

Katika ‘media tour’ hii yake, Weezdom amekuwa akiulizwa maswali mbalimbali na yeye hajakuwa mchoyo wa kutema nyongo, rah asana!

Juzi akiwa katika stesheni moja ya redio nchini, Weezdom amezungumzia sababu zilizomfanya kubwaga manyanga katika kueneza injili kwa nyimbo na kujibwaga kwenye mitindo ya kidunia.

Weezdom alisema kwamba wasanii wa injili walimtenga kwa kile anasema kwamba ni kuwa na watoto wengi nje ya ndoa, hata kumzidi ‘baba yake’ katika muziki wa injili, nazungumzia Bahati wa rekodi lebo ya EMB.

“Watu wa gospel walifeel mimi sifai kuwa mmoja wao, lakini niulize, yaani uko na mtoto mahali, ni dhambi ijulikane uko na yeye? Unaishi na mtoto wako kwa siri kwa sababu ya kazi, ati ndio uitwe hapa isijulikane uko na watoto. So wakati walijua mambo yangu, wakaanza kunitoa kwa vitu vingi sana. Ndio maana mimi nilijitoa. Niko na watoto wanne na sasa sifanyi muziki wa gospel tena kwa sababu nilipigwa marufuku kuna kanisa na stesheni siwezi taja, walinipiga marufuku kuenda huko kwa sababu nina watoto,” alisema Weezdom.

Alisema kwamba licha ya kuwa na watoto hao wote na kina mama tofauti tofauti, yeye bado anashirikiana nao vizuri kwa malezi hata kama wote hao wako katika mahusiano na watu wengine.