"Mylee alisema kuna 'mubaba' alimpa ofa ya Range Rover, nikamuacha" - Weezdom

Muhtasari

• Weezdom amesema kwamba aliamua kukatisha mahusiano na mpenzi wake wa muda mrefu Mylee Stacey kwa sababu mwanadada huyo alifunguka fikira zake katika mahojiano moja na kusema kwamba anafikiria kukubali ofa ya kununuliwa Range Rover na 'mubaba'

Weezdom, Stacey Mylee
Image: Maktaba

Msanii Weezdom ni gumzo la mitandaoni kwa takribani wiki mbili sasa baada ya kuachana na mpenzi wake wa muda, Mylee Stacey na kuanza kuchambana mitandaoni huku msanii huyo alizindua penzi lake kwa mwanamitindo Manzi wa TRM.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na watangazaji Mwende na Clemmo ambapo waliandamana na mpenzi wake mpya Manzi wa TRM, Weezdom amefunguka kuhusu kile kilichosababisha mahusiano yake na Stacey kufikia hatua ya kutorekebika kwa mara ya mwisho kabisa baada yao kucheza mchezo wa kuachana na kurudiana kwa muda mrefu hapo awali.

Weezdom alisema kwamba sababu kuu ya kuachana ilikuwa ni matamshi ya Stacey kwenye interview na watangazaji hao mwezi mmoja uliopita ambapo mwanadada huyo alisema kwamba alikuwa amepokezwa ofay a kununuliwa gari aina ya Range Rover na mwanaume aliyemzidi umri na ambaye alimtaka kimapenzi, mitaani wanasema ni ‘mubaba’ na kwamba alikuwa anatathmini kukubali ofa hiyo.

Weezdom alisema kwamba Stacey alitamka maneno hayo wakiwa Pamoja kwenye mahojiano hayo na jambo hilo lilimkwanza sana ndani kwa ndani lakini akajitia shime kiume na jioni hiyo walipofika nyumbani mambo hayakuenda sawa tena kwani huo ndio ulikuwa mwanzo wa nyufa kuonekana hadharani baina yao kwa mara ya mwisho kabisa.

“Kwa kumuuliza lile swali, nyinyi ndio mlisababisha na hiyo jioni vitu hazikuwa poa. Nafeel tu nimuache aexplore life kwa watu wengine kwa sababu yeye ni kama anafeel mali ndio kila kitu, lakini kwangu mimi mapenzi ndio kila kitu,” alisema Weezdom huku akiwarushia lawana watangazaji hao kimzaha.

Weezdom pia alifichua kwamba wamekuwa marafiki kwa muda mrefu na mpenzi wake mpya Manzi wa TRM na kusema kwamba hata walipokuwa wakikorofishana na Stacey katika mahusiano yao, Manzi wa TRM alikuwa mara nyingi analivalia njuga suala hilo na kutoa ushauri nasaha kwa Stacey jinsi ya kumhendo mwanaume.

“Sai mimi niko happy niko na my best friend, eeh! Hata siamini tunaitana beb,” alisema Weezdom.

Msanii huyo pia alipuuzilia mbali madai kwamba ni kiki tu wanatafuta mitandaoni na Manzi wa TRM na kusema kwamba yeye katika maisha yake hajawahi fanya kiki na mwanadada ili kufukuzia umati kwenye mitandao ya kijamii.