Hatimaye Diamond aweka wazi kirefu cha EP ya #FOA

Muhtasari

• Hatimaye msanii Diamond ameweka wazi maana ya jina la EP yake ya FOA  inayotarajiwa kutoka Machi 11.

Diamond Platnumz
Image: Instagram

Hatimaye msanii Diamond Platnumz ameweka wazi kirefu cha EP yake ambayo mwishoni mwa wiki jana aliitangaza kwa kutoa kifupi chake kuwa FOA.

Diamond ametangaza Jumatatu kwamba kirefu cha jina la EP yake ambayo inatarajiwa kutoka Machi 11 ni First Of All, kwa maana kwamba ni Kabla ya Yote, wengi wakisema maana hii inaonesha uhalisia wenyewe kwani ni EP yake ya kwanza kabisa tangu aingie kwenye muziki Zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Wiki jana Diamond alipakia picha za kifupi cha jina la EP hiyo ambayo ilitembezwa mitandaoni chini ya alama ya reli ya #FOA na kuwataka wafuasi wake na mashabiki wake kung’amua kirefu chake ambapo wengi walitatizika kichwa kwa ubashiri tofauti tofauti za kuchekesha na zingine za kukejeli.

Lakini almradi wenye midomo walishasema kwamba hata usiku uwe mrefu vipi bado kutapambazuka tu, basi Jumatatu kulipambazuka na msanii huyo akalitatua hilo kwa kuweka wazi kirefu chake.

Kinachosubiriwa na wengi sasa ni kujua idadi ya ngoma ambazo EP hiyo inasheheni lakini hili bila shaka litabainika tarehe 11 mwezi huu ambapo pia wengi wanatarajia kuipata radha kamili na iliyotukuka ya muziki wa nguli huyo wa bongo fleva kama ilivyokuwa kawaida yake miaka ya nyuma.