Bakhresa hatongozi wafanyakazi - Harmonize ampiga vijembe Diamond

Muhtasari

• "Bakhresa hana hulka ya kutembea na wafanyakazi" - Harmonize aliandika baada ya tetesi za Diamond kutoka kimapenzi na Zuchu

Harmonize na Diamond
Harmonize na Diamond
Image: INSTAGRAM

Msanii Harmonize anaendeleza kumchimba mikwara msanii ambaye ni kama baba yake kimuziki, Diamond Platnumz.

Katika wimbo wake mpya ambao amekuwa akiuahirisha kwa muda ili uoane na EP ya FOA ya Diamond, Harmonize hatimaye wikendi iliyopita aliachilia kibao hicho alichokitaja kuwa cha mwaka na kukipa jina Bakheresa.

Baadhi ya maudhui katika ngoma hiyo yanamlenga moja kwa moja msanii Diamond ambapo anaeleza kwamba Bakhresa hana mazoea ya kutoka kimapenzi na wafanyikazi, kipande ambacho kinamlenga Platnumz ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa akisemekana kutoka kimapenzi na Zuchu ambaye ni kama mfanyikazi chini ya lebo yake ya Wasafi.

Harmonize baadae alienda kwenye instastories zake akielezea sifa za Bakhresa kuwa ni mchapakazi na hana hulka ya kutongoza wafanyikazi wake, jambo lililotajwa kuwa ni kumfuma Diamond vijembe.

Sifa ya Bakhresa ni mchapakazi…!!! Hachagui biashara hadi tui la nazi…!!! Anaamini mafanikio ni hatua kama kupanda ngazi…!!! Bakhresa hana hulka ya kutembea na wafanyakazi…!!! Matajiri hawana time kuongea…!!! Lini ulishasikia Bakhresa anazungumza umbeya…” aliandika Harmonize

Hili linakuja siku moja tu baada ya Diamond kuonekana kumchamba Harmonize kwenye wimbo wake mpya wa Nawaza ambapo anasema kwamba binadamu hawana wema kwani unamkuza mtoto anakuja kukutakia mabaya ukubwani akimlenga Harmonize ambaye alimtoa kimuziki na kisha baadae akaja kuwa adui wake mkubwa hata zaidi ya Alikiba.

“Nimejifunza binadamu kweli hawana jema, yaani mtoto unayemtunza ndiye anakuombea ukilemam, nashangaa,” kipande cha wimbo huo wa Diamond kinasema.