Rayvanny aingia #GoldenClub, atinga streams 100M Boomplay

Muhtasari

“Najivunia kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika mashariki kufikisha streams milioni 100 kwenye jukwaa la Boomplay" - Rayvanny

Mkurugenzi mkuu wa lebo ya Next level Music, Rayvanny
Mkurugenzi mkuu wa lebo ya Next level Music, Rayvanny
Image: instagram

Staa wa bongo fleva na mkurugenzi mkuu wa rekodi lebo mpya kabisa ya Next level Music, Rayvanny anazidi kuvuma kote baharini na nchi kavu.

Msanii huyo hakawii kuvunja na kuandikisha rekodi mpya katika tasnia ya muziki si tu nchini Tanzania bali katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika kwa jumla, kwani anazidi kutangaza uwepo wake kwa herufi kubwa za dhahabau tena kwa njia ya kifalme zaidi.

Jumatatu msanii huyo alisherehekewqa na jukwaa kubwa la kupakua miziki la Boomplay kwa kuwa msanii wa kwanza kabisa kuwahi kutokea katika ukanda wa Afrika Mashariki kufikisha ‘streams’ milioni 100 za miziki yake.

Yaani hata nguli wa miziki, Diamond Platnumz licha ya ukali wake katika muziki mpaka kujiita Simba kwa jina la kimajazi lakini bado hajawahi vuma kiasi hicho cha kufikisha streams milioni 100 kwenye Boomplay.

Akisherehekea ushindi huo, Rayvanny aliwashukuru mashabiki wake kote ulimwenguni kwa kumwezesha kufika hatua hiyo kubwa na kukaribishwa kwenye kikundi cha Golden Club, kikundi ambacho ni cha wasanii wenye wamegonga streams milioni mia kwenda mbele kwenye Boomplay.

“Najivunia kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika mashariki kufikisha streams milioni 100 kwenye jukwaa la Boomplay. Ahsante sana kwa mashabiki wangu kote ulimwenguni na pia shukrani kubwa kwa Boomplay,” aliandika Rayvanny kwenye Instagram yake.

Msanii huyo sasa anatamba kwenye kundi la Golden Club na mastaa kutoka bara la Afrika kama Davido, Joeboy, Omah Ley, Fireboy ambao wote wanatokea Magharibi mwa Afrika.

Hongera Chui!