"Wewe ni mshirika wangu wa kitandani" Simon Kabu amwambia mkewe wakiadhimisha miaka 13 ya ndoa

Muhtasari

• Wajasiriamali Simon Kabu na Mkewe waliadhimisha miaka 13 katika ndoa yao huko kwenye kisiwa cha mauritius.

• Wawili hao walimlipia nauli ya ndege mcheza densi Moya David kwa ajili ya kucheza densi na kuufikisha ujumbe wa Simon kwa mkewe.

Simon Kabu, mkewe Sarah Kabu na watoto wao
Image: Simon Kabu (Facebook)

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya utalii ya Bonfire Adventures Sarah Kabu ni mmoja kati ya wanawake wenye furaha ya ndoa baada ya mumewe ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Simon Kabu kumtungia mishororo mitamu ya mahaba walipokuwa wanasherehekea kuadhimisha miaka 13 ya ndoa iliyostawi.

Wawili hao waliadhimisha miaka kumi na mitatu ya ndoa katika kisiwa cha Mauritius na Simon aliamua kumfanyia mkewe bonge la shtukizo kwa kumtumia ujumbe huo uliojawa maneno ambayo kila mtu mwenye ari ya kuingia kwenye mahaba angependa kusikia kila siku ya kalenda.

Simon Kabu alimhakikisha maadhimisho hayo yanakwenda mbele sawasawa na hivyo aliifanya zaidi ya matajrajio ya mkewe kwa kumlipia tikiti ya ndege mcheza densi maarufu kwenye mtandao wa TikTok Moya David kusafiri nao hadi kisiwa hicho kilichopo Bahari Hindi ili kucheza densi zake na kuufikisha ujumbe huo kwa mkewe kwani yeye mwenyewe aliona hangeweza kuufikisha ujumbe kwa njia nzuri zaidi na anavyofanya Moya David.

Katika ujumbe huo wa kimahaba ambao Moya David alikuwa na fursa ya kuusoma kwa maskio ya Sarah Kabu ambaye maskio yake yalikuwa yametega antenna kisawasawa, Simon alimsifia kuwa mke bora katika miaka yote 13 ambayo wamekuwa mwili mmoja na kufanikisha mambo mengi likiwemo kumiliki kampuni kubwa ya utalii nchini Kenya.

“Sarah… Miaka 13 iliyopita, siku kama leo… kwenye ufuo wa Ziwa Naivasha, sote tuliifanya! Imekuwa miaka 13 ya kujitolea, kujituma, kufanya kazi kwa bidii na busara na muhimu zaidi baraka za Mungu kuanzia kwa watoto, biashara na ushirikiano. Tunaposherehekea kuadhimisha siku hii fahamu tu kwamba, Wewe si mshirika wangu tu katika vile vitendo bali pia ni mama wa watoto wangu, biashara na mshirika wangu wa kitandani. Mshangao baada ya mshangao… Huenda tukaondoa jino letu la mwisho pamoja,” Moya David aliusoma ujumbe huo wa kimahaba kwa mkewe Simon Kabu na kufanya uso wake kung’aa ghafla.

Ikumbukwe hata kama wapenzi hao wawili ambao pia ni wajasiriamali wamedumu kwenye ndoa yao miaka zaidi ya mwongo mmoja, haijakuwa mserereko kama ambavyo wengi walidhani, kwani hivi majuzi tofauti zao zilidhihirika wazi na nyufa kubwa kuonekana iliyotishia kusambaratisha ndoa yao hiyo ya miaka mingi pale ujumbe wa WhatsApp ulipovujishwa kwamba Sarah Kabu anamtuhumu mumewe Simon na kumuita katili.

Lakini Simon Kabu alitumia busara za kiume na kuliendea Sakata hilo kwa mwendo wa pole ambapo alifanikiwa kuirudisha ndoa yake pamoja kinyume na matarajio ya wengi waliokuwa wameanza kunong’ona kwamba ni mwisho wa reli katika safari yao ya mapenzi.

Hongereni Kabus!