Msanii Kusah asherehekea ngoma yake kufikisha views 10M, "Ilikuwa ni ndoto yangu"

Msanii Kusah alisema kwamab alipoanza muziki watu wengi hakuwa wanamuaminia.

Muhtasari

• “Wengi walikua wakidhani kwamba huwezi kufika kokote bila kuwa chini ya Boss, Label au Watu wenye nguvu kubwa" - Kusah

Nchini Kenya kwa muda mrefu wasanii wamekuwa wakionekana washamba kwa kusherehekea hatua kama vile ngoma zao kufikisha idadi fulani ya watazamaji kwenye mtandao wa YouTube.

Ila unaambiwa nchini Tanzania ni zaidi ya hapo kwani wasanii wengi ngoma kufikisha watazamaji milioni moja Kwenda mbele ni ndoto ya wasanii wengi sana katika ukanda huu ambao ndio mwanzo unakua kimuziki na kuzidi kugundua majukwaa mengine ya kusukuma miziki kando na YouTube ambayo imejulikana kwa muda mrefu kuwa jukwaa bora na wasanii wa Afrika Mashariki.

Msanii wa hivi karibuni kutisha na kusimamisha mitandao ya kijamii ni msanii Kusah kutoka Tanzania ambaye baada ya ngoma yake ya ‘I Wish’ kufikisha watazamaji milioni 10 kwenye mtandao wa YouTube.

Kusah alisherehekea na kusema kwamba hiyo ilikuwa moja kati ya ndoto zake kuona ngoma yake inagonga watazamaji mamilioni na kumshukuru Mungu kwamba mwisho wa siku ndoto yake imetimia, miezi tisa tu tangu kuiachia video hiyo kali.

“Zilikuaga Ndoto Zangu za Kila Siku Hatimae Mungu Ametenda na Kunifundisha Kwamba kila kitu kinawezekana. Kwa upande wangu hii ni kubwa saana 10million Views ndani ya miezi 9” alisherehekea Kusah.

Msanii huyo alizidi kusema kwamba si kila mtu aliyekuwa anamuaminia katika safari yake ya kimuziki kwani wengi walikuwa wanasema hawezi fika popote lakini hatua hii imewapiga changa la macho wale waliokuwa na dhana kama hiyo.

“Wengi walikua wakidhani kwamba huwezi kufika kokote bila kuwa chini ya Boss, Label au Watu wenye nguvu kubwa haswa Ila Kwa sasa imekua tofauti kizuri Ndio hupendwa,” alisema Kusah kwa furaha kubwa.

Vile vile, msanii huyo alichukua fursa hiyo kutoa neno na kuhimiza kwa wasanii wanaochipukia kwenye gemu la muziki na kuwaambia kwamba nafasi ni nyingi bora msanii unafanya muziki wa kuvutia

 “Wadogo zangu, kaka na dada zangu ambao ndio mmeingia kwenye industry niwaambie tu kwamba nafasi ni nyingi na kila kitu kinawezekana ukiamua. Asanteni saana watu wangu,” Kusah alishukuru kwa furaha nyingi.