Jalang'o awapa wafanyikazi wa Jalang'o TV hisa za 80% naye kubaki na 20%

Alisema kwamab sasa wao ndio watakuwa wanamlipa asilimia 20 ya mapato kila mwezi

Muhtasari

• "Hii sasa nimewaachia mtafute mahojiano na kufanya mambo mengi kwa sababu pale ninakoenda mimi nitakuwa na majukumu mengi,” Mbunge huyo mpya wa Lang’ata alisema.

Mbunge mteule wa Lang'ata Phelix Odiwuor
Mbunge mteule wa Lang'ata Phelix Odiwuor
Image: Screengrab//Youtube

Mbunge mteule wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o ametangaza kuachia hisa za chaneli yake ya YouTube kwa vijana ambao walikuwa wanafanya kazi na yeye katika kuikuza chaneli hiyo.

Jalang’o ambaye ndiye muasisi wa Jalang’o TV kwenye mtandao wa YouTube alitangaza kwamba kutokana na majukumu mengi ambayo yanamsubiria mbeleni kama mbunge, hatoweza kuwa na muda wa kutosha kuendesha shughuli za kawaida za chaneli hiyo kama kutafuta mahojiano na watu mashuhuri na hivyo atawaachia majukumu yote mia kwa mia vijana wake.

Aliwaambia kwamba ataibadilisha umilisi wa akaunti za malipo ili mapato yote sasa yawe yanaenda kwa akaunti ambayo vijana hao wanafungua na faida ya hisa asilimia 80 itakuwa yao kila mwezi huku Jalang’o akipokezwa dau la asilimia 20 pekee ya mapato yote kila mwezi.

“Hii chaneli nataka sasa niitoe kwa akaunti zangu za malipo, pesa zisiwe sasa zinaingia kwangu. Nataka mfungue akaunti ili pesa zote zikuwe zinaingia kwenu na mimi kila mwezi mtakuwa mnanilipa 20% ya mapato yote ambayo mtakuwa mmekusanya. Hii sasa nimewaachia mtafute mahojiano na kufanya mambo mengi kwa sababu pale ninakoenda mimi nitakuwa na majukumu mengi,” Mbunge huyo mpya wa Lang’ata alisema.

Mchekeshaji Jalang’o alimbwaga mbunge wa sasa Noxon Korir aliyekuwa anajaribu kutetea kiti chake kupitia chama cha UDA huku Jalang’o akiwania kwa tikiti ya ODM ambapo Korir alikubali matokeo mapema hata kabla ya IEBC kutangaza rasmi matokeo ya uchaguzi katika eneo bunge hilo lililopo viungani mwa mji mkuu wa Nairobi.