“Mabinti wengi wananitaka, wananimezea mate, mimi naringa!" - Stevo Simple Boy

Msanii huyo alisema DM yake imefurika mabinti

Muhtasari

• Mabinti wengi Wananimezea mate. Kuna wale pia wanataka umaarufu, na pia kuna wale wanataka hela - Stevo.

Msanii huyo amesema wanawake wengi wanamtaka ila anaringa
Stevo Simple Boy Msanii huyo amesema wanawake wengi wanamtaka ila anaringa
Image: Instagram

Mwanamuziki Stevo Simple Boy amefichua kwamba tangu amvishe kichuna wake pete hadharani takribani mwezi mmoja uliopita, DM yake imefurika na mabinti wengi wanaomtaka kimapenzi.

Akizungumza na mkuza maudhui Presenter Ali, Stevo Simple Boy alisema kwamba mabinti wengi wanamtolea macho ya kumtaka kimapenzi lakini akadokeza kwamba yeye amejifunza kukaa ngumu na kuwaringia kwani hawataki.

Simple Boy alisema kwamba katika hao wote ambao wanamtaka, kila mmoja ana lengo lake kivyake. Kuna wale wanaotaka umaarufu kupitia kwake, kuna wale wanaotaka kumchuna kimfuko na wengine nia zao zinatofautiana na hazijulikani.

“Mabinti wananitaka, mimi naringa. Mabinti wengi Wananimezea mate. Kuna wale pia wanataka umaarufu, na pia kuna wale wanataka hela. Kuna wale wanataka kuwa na mimi wajibambe. Na pia kuna wenye wako na hayo mapenzi ya ukweli. Shida inatokea kujua yule mwenye ako na mapenzi ya ukweli,” Simple Boy alisema.

Msanii huyo baada ya kutengana na mpenzi wake wa muda mrefu, mwanamitindo Pritty Vishy, alimvisha mchumba mpya kwa jina Gee pete ya uchumba na hivi karibuni katika mahojiano ya kipekee alisikika akisema kwamba ana mipango ya kufunga ndoa na kutulia kabisa.

Aliyasema hayo licha ya mkanganyiko unaozunguka mahusiano yake na Gee ambapo jamaa mmoja anayedai kuwa msanii chipukizi kwa jina Rapdon kujitokeza na kumuonya Stevo Simple Boy kwamba binti huyo ni mpenzi wake na kumtaka akae mbali naye.