Tundaman: Rayvanny nilimsaida ila hajawahi kunisaidia, Harmonize ashawahi kunipa 10M

Tundaman alisema ulikuwa uamuzi wake kutaka collabo ya Badman kuwekwa YouTube ya Harmonize kama kurudisha fadhila.

Muhtasari

• Harmonize kupata haniumizi mimi, sasa hivi nikimwambia Harmonize nina shida ya milioni 10 atanipatia - Tundaman.

Tundaman amsifia Harmonize kuwa mtu mzuri huku akimkandia Rayvanny kuwa hajawahi kumsaidia
Tundaman amsifia Harmonize kuwa mtu mzuri huku akimkandia Rayvanny kuwa hajawahi kumsaidia
Image: Instagram

Msanii mkongwe katika Sanaa ya Bongo Fleva, Tundaman amezungumzia makubaliano yake na msanii Harmonize na kueleza kwa kina ni kwa nini alikubali ngoma yake collabo iwekwe kwenye akaunti ya YouTube ya msanii huyo wa Konde Gang.

Tundaman pia alizungumza kwa hisia kwamba katika safari yake ya muziki ambayo haijaanza jana wala juzi, amewahi kuwasaidia wasanii kama Rayvanny na Dogo Janja na kwa sasa wana mkwanja mrefu lakini hata siku moja hawajapata kumsaidia.

Alisema Harmonize alimsaidia pakubwa kwa kusimamia kila kitu katika collbao – Badman ambayo alimshirikisha na ndio sababu aliamua pia kurudisha fadhila kwa kumkubalia kuipakia kwenye akaunti yake.

Makubaliano yake na Harmonize yalikuwa kwamba yeye auze ngoma ile ikiwa kama sauti tu kwenye majukwaa mbali mbali na kama njia moja ya kurudisha shukrani kwa Harmonize, basi amkubalie kupakia video yenyewe.

“Alisema nisitoe hela ya video, akasimamia yeye, kila kitu mpaka mavazi kweney video na gari na akaipromoti kama ngoma yake, nikaona nitamsaidia vipi, ndio nitasema achukue video na kuiweka kwenye YouTube yake kwa sababu ana ufuasi mkubwa na imeenda sana kama ambavyo nilikuwa nategemea. Mimi sikuangalia Napata nini au nakosa nini kwa sababu alichokitoa yeye alikitoa kwa moyo mmoja,” Tundaman alisema.

“Mimi sijali, nimemsaidia Dogo Janja ana mahela mengi hanisaidii, nimemsaidia Rayvanny vile vile ana mihela mirefu hanisaidii,” Tundaman alifunguka.

Alisema yeye hata kama harmonize anafaidika kutokana na ngoma ile si kitu kibaya kwani amewahi kumsaidia katika matukio mbali mbali.

“Harmonize kupata haniumizi mimi, sasa hivi nikimwambia Harmonize nina shida ya milioni 10 atanipatia kwa sababu amewahi kunipatia. Ni mtu anayeishi maisha fulani ya ujamaa sana,” Tundaman alimsifia tajiri wa Konde Gang.