Maoni: Harmonize ana uwezo mkubwa wa kufikia mafanikio ya Diamond

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Diamond ni namba 2, Alikiba namba 6 na Harmonize namba 8.

Muhtasari

• Diamond ndiye Tajiri namba mbili katika ukanda wa Afrika mashariki, nyuma ya msanii na mwanasiasa Bobi Wine kutoka Uganda.

Diamond ana mafanikio makubwa kutokana na kujiuza vizuri - mdau
Diamond ana mafanikio makubwa kutokana na kujiuza vizuri - mdau
Image: Instagram

Baadhi ya wadau wa muziki nchini Tanzania wanahisi kwamba wasanii Harmonize na Rayvanny ndio kidogo walio na uwezo wa kufanya udhubutu wa kufikia utajiri na mafanikio ya msanii Diamond Platnumz katika muziki.

 Mdau HopeTyga anasema kwamba kwa sasa, Diamond ndiye Tajiri namba mbili katika ukanda wa Afrika mashariki, nyuma ya msanii na mwanasiasa Bobi Wine kutoka Uganda na mshindani wake wa muda wote Alikiba ni namba sita huku Harmonize akiwa nambari 8.

Kulingana na mdau huyu, itakuwa vigumu sana kwa wasanii wengine katika vizazi vijavyo kufikia hatua zile ambazo Diamond amefika ila akasema baadhi yao kama Harmonize na Rayvanny wana nafasi kubwa ya kumfikia kwa kile alisema kwamba wapo katika mkondo mzuri endapo wataendelea kukaza buti.

Ni vigumu sana wasanii wengine kufika Level za Diamond Platnumz. Wasanii ambao kidogo kwa hapo badae wanaweza kufikia utajiri wa Diamond ni Harmonize au Rayvanny maana wana misingi mizuri, ila wengine itakuwa vigumu sana,” aliandika.

Alisema kigumu ambacho kinawakwamisha wasanii wengine ni kushindwa kujiuza vizuri kibiashara kaam ambavyo Diamond anafanya na wengi hujikita katika misingi ya kufanya miziki ya kufurahisha na kuburudisha ilhali Diamond anachukulia muziki kama biashara.

“Njia alizopita Diamond wengi hawapiti, wasanii hawajui kuji-brand kibiashara. Kilichomtajirisha Diamond ni Branding. Ame-brand Vizuri neno "Wasafi" ndio maana amepata Business Partners. Kwa asilimia kubwa utajiri wa Diamond umetokana na Biashara ya Lebo, Media.  Wasanii wamekaa kizembe mno hawana akili ya biashara wanawaza kupata laki laki za Show,” Tyga alisikitika.

Mdau huyo aliwasifia baadhi ya wasani wenye wamejiweka katika mkondo mzuri kibiashara na kutumia umaarufu wao vizuri ili kujiongezea kipato kando na muziki.

“Kwasasa Pongezi kubwa ziende kwa Diamond, JUX, Vanny, Harmo hawa wanajua kujiongeza,” Alisema.