Familia ya Diamond yaukubali wimbo wa Alikiba, mama na dadake waupakia mitandaoni

Mamake Diamond Pamoja na dadake Esma wote walionekana kuufurahia wimbo huo

Muhtasari

• Napendwa ndio jina la wimbo huo ambao Alikiba alishirikishwa na Mocco Genius.

Familia ya Diamond Platnumz imeukubali wimbo wa Alikiba
Familia ya Diamond Platnumz imeukubali wimbo wa Alikiba
Image: Moses Sagwe art

Mzalishaji wa muziki kutoka nchini Tanzania, Mocco Genius miezi michache iliyopita alitangaza kuanza safari yake kama msanii wa Bongo Fleva baada miaka kadhaa kuwazalishia miziki makumi ya wasanii wa Bongo.

Mwezi mmoja hivi uliopita, Mocco alikuja akaachia kibao chake cha kwanza kabisa kwa jina ‘Napendwa’ na kibao hicho baadae Mocco alimshirikisha nguli wa shughuli hizo wa muda mrefu, Ali Kiba katika remix ambayo imepaisha namba pamoja na mapokezi ya wimbo kiujumla.

Kilichowashangaza wengi ni baada ya klipu fulani kuibuliwa mitandaoni familia ya msanii Diamond Platnumz kwa maana ya dadake Esma Khan na mamake Bi Sandra au mama Dangote wakiufagilia sana wimbo ule huku wakiutizama kwenye runinga.

Katika klipu hiyo, mama Dangote wanaonekana wakiwa na bintiye Esma wakiutazama wimbo wa Alikiba na Mocco kwenye runinga huku Esma akisema kuwa mamake anaupenda wimbo ule mwanzo mwisho.

“Jamani huyu mama aipenda hii nyimbo, anaipenda sana jamani,” Esma Platnumz anasikika akiongea huku mamake akionekana anairekodi video ile iliyokuwa inacheza runingani kwa kutumia simu yake.

Familia ya Diamond Platnumz
Familia ya Diamond Platnumz
Image: Moses Sagwe art

Mocco Genius katika mahojiano alipoulizwa hisia zake kuhusu ile klipu, alisema kuwa alijawa na faraja sana kwa kuona Mamake Diamond anaufagilia wimbo wake na kuwa suala hilo lilimtia moyo sana.

Aliweka wazi kuwa hata Diamond Platnumz mwenyewe alimandikia ujumbe wa kumwambia kwamba remix ile ilikuwa kubwa sana na yenye mistari ya kukosha kutoka kwake na kwa Alikiba.