Esma Platnumz amshauri Diamond kuwakutanisha watoto wake wote

Alisema hatua hiyo itawafanya kujenga mapenzi ya udugu tangu wakiwa watoto na kujuana pia.

Muhtasari

• Diamond alikuwa amekataa mbele ya wanawe na Zari kuwa hana watoto wengine kando na hao.

• Hatua hii ilimchukiza Esma ambaye alisema msanii huyo amewakosea watoto wao vibaya mno kwa kuwaficha.

Esma achukizwa na Diamond kutowaambia watoto ukweli
Esma achukizwa na Diamond kutowaambia watoto ukweli
Image: Instagram

Wiki jana baada ya msanii Diamond Platnumz kupakia klipu ambayo watoto wake walikuwa wanamuuliza maswali makali pamoja na mzazi mwenziwe, Zari, sasa dadake anahisi msanii huyo alikosea katika baadhi ya majibu yake kwa watoto.

Katika video hiyo ambayo Diamond alipakia na kudokeza kwamba aliitembelea familia hiyo yake katika nyumba ya Zari nchini Afrika Kusini, na watoto wao wawili, Nillan na Tiffah wakawaita kwenye kikao sebuleni na kuanza kuwauliza maswali makali, Diamond alistaajabu kwamba wanawe wana upeo mkubwa sana wa kung’amua maneno, mbali na alivyokuwa anawafikiria.

Katika moja ya matukio kwenye klipu ile, watoto hao wawili walionekana kumtetea baba yao huku wakimlaumu Zari kwa kusababisha mahusiano yao kusambaratika na sasa wanaishi mbali na baba yao mzazi – Diamond Plarnumz.

Walionekana kutoona doa hata kidogo kwa baba yao na hata kumtetea dhidi ya maneno ya Zari kuwa ana watoto wengine na wanawake wengine kando na yeye.

Kwa haraka haraka tu ni kwamba msanii huyo ana watoto wengine wawili wa kiume amabo mmoja alizaa na mwanamitindo Hamisa Mobetto na mwingine akazaa na aliyekuwa mtangazaji na ambaye sasa ni mwanamuziki kutoka Kenya, Tanasha Donna.

Hatua ya Diamond kutowaelezea watoto wake na Zari kuwa wana ndugu wengine kando na wao ilionekana kumkera dadake, mjasiriamali wa vijora na madera, Esma Platnumz.

Kupitia chapisho hilo la Diamond, Esma alionesha kutoridhishwa kwake na kumlaumu Diamond kuwa alikosea kutowaelezea watoto kuhusu uwepo wa ndugu zao wengine na hata ikiwezekana awakutanishe na kujuana.

Alionekana kudokeza kwamba pakubwa angewaelezea kuhusu ndugu yao, ambaye ni mtoto Diamond alizaa na Tanasha Donna, Naseeb Junior ila hakumtaja mtoto wa Hamisa Mobetto.

Umewakosea watoto ulitakiwa uwaambie kuna Tom kaka pia ndugu yao ili wajenge mapenzi tangu wakiwa wadogo kama vipi wakutane nae pia,” Esma alionesha kutoridhishwa kwake na hatua ya Diamond kukataa mbele ya watoto wake kuwa ana watoto wengine nje.