Trio Mio asema yuko huru kupiga sherehe baada ya kufikisha miaka 18

Hatimaye nimeingia kwenye kundi halali kisheria - Trio Mio.

Muhtasari

• Nimekuwa tu na umri wa miaka 18 leo marafiki zangu na naskia wah! 😁 Tuzidi kuzidi katika safari hii pamoja - Trio Mio.

Trio Mio ahserehekea miaka 18
Trio Mio ahserehekea miaka 18
Image: instagram

Mwanamuziki maarufu wa miziki ya Gengetone humu nchini Trio Mio Jumamosi alifikisha miaka 18 na kujisherehekea kwa njia maalum.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Trio Mio alidhihirisha furaha yake akisema kwamba hatimaye amefikisha umri wa kuhalalishwa kufanya kitu chochote kwani miaka 18 ndicho kigezo cha kumtambua mtu kama mzima ambaye hawezi kuzuiliwa kutoka kufanya baadhi ya masuala.

“Hatimaye nimeingia kwenye kundi halali kisheria! 🎉🎉   Nimekuwa tu na umri wa miaka 18 leo marafiki zangu na naskia wah! 😁 Tuzidi kuzidi katika safari hii pamoja,” Trio Mio aliandika.

Msanii huyo mchanga zaidi katika tasnia ya muziki wa humu nchini na ambaye amepata mafanikio makubwa tangu kutia guu kwenye gemu la muziki nchini, aliwashabiki ndugu zake na mama yake kwa kusimama naye siku zote na muda wote katika kuhakikisha kwamba anaweka sawa mambo yake kimuziki lakini pia kielimu, kwani bado angali mwanafunzi.

“Namshukuru Mungu, mama yangu kwa kumzaa huyu pikin mzuri 😂 dada zangu kwa kuwa karibu nami kila wakati, kaka yangu kwa kuwa ngao yangu, timu yangu kwa kazi nzuri tunayofanya na ninyi mashabiki wangu kwa kushikamana nami kupitia ukuaji wangu kama msanii,” Trio Mio aliandika kwa furaha.

Kando na hapo, aliwaahidi mashabiki wake kwamba maadamu sasa amefikisha umri halali wa kupiga sherehe na tafrija kokote, anarudi na ukali wa moto wa jangwani usiomithilika.

Alisema kwamba Desemba hii anatarajia kumaliza mtihani wake wa shule ya upili na kuahidi kwamba tasnia ya muziki anakuja kuiteka kijeshi.

“Kijana ako 18 na namaliza mtihani Desemba, mistake kujua vile nitakuja na ubaya. Zawadi kubwa mtakayonipa nikisherehekea miaka 18 ni kuitazama ngoma yangu mpya #HapaKaziTu,” Trio Mio alisema huku akizungumzia pia ngoma yake mpya.

Wasanii mbali mbali walimsherehekea na wengine kumkaribisha kwenye umri halali rasmi huku wakiahidi kumshika mkono hata zaidi ili kufanikisha ndoto zake kimuziki kwani bado ni mchanga kiumri.

“Karibu kwa Utu Uzima 😁😁💪🏾💪🏾.. uko tayari kwa hilo. Happy birthday fam... Maliza shule utese vizuri,” msanii mkongwe, Nameless alimhongera.

Wengine walimfananisha na msanii nguli marehemu E-Sir na kusema kwamba kupitia yeye huwa wanaona kama ni mwendelezo wa msanii huyo anayeshabikiwa mpaka leo hii, miaka 19 tangu kifo chake.

“Inashangaza jinsi ulivyozaliwa mwaka mmoja baada ya Legendari Esir kufa. Na kuona picha hii, kuna kufanana kati yenu wawili. Tulipoteza Hadithi moja na Tulipata Nyuma nyingine mara moja. Ni mpito mkamilifu kama nini, au ni, "kuzaliwa upya"” shabiki kwa jina Swir Nyar Kano alimwambia.