Mbosso akwepa ushindani wa kibabe dhidi ya Harmonize, alazimika kubadili tarehe ya EP

Mbosso alikuwa ametangaza kuachia EP yake Oktoba 28, tarehe ambayo pia Harmonize aliikomalia kuachia albamu yake.

Muhtasari

• Alhamisi hii Oktoba 27 nitakuwa nazindua rami EP yangu katika fukwe za Barra Beach TZ kuanzia saa kumi na mbili jioni - Harmonize.

Harmonize na Mbosso
Harmonize na Mbosso
Image: instagram

Msanii kutoka lebo ya WCB Wasafi, Mbosso Khan amekwepa ugomvi na ushindani wa kibabe na Harmonize kimtindo baada ya kubadilisha tarehe yake rasmi ya kuachia albamu yake fupi kwa jina Khan.

Kupitia ukurasa wake, awali Mbosso alikuwa ametangaza kuwa EP yake hiyo ingetoka Ijumaa ya Oktoba 28 ila akalazimisha kubadilisha tarehe hiyo na kutangaza upya baada ya Harmonize kuikoromea Oktoba 28 pia kuwa siku ya kuachia rasmi albamu yake kamilifu, kwa jina Made For Us.

Jumatano jioni, Mbosso alipakia majina ya watu mashuhuri wengi tu ambao wamealikwa kuhudhuria uzinduzi wa EP yake ya Khan na kutangaza kwamba itatoka Oktoba 27 na si Oktoba 28 kama alivyoweka wazi tangu hapo awali.

“Alhamisi hii Oktoba 27 nitakuwa nazindua rami EP yangu katika fukwe za Barra Beach TZ kuanzia saa kumi na mbili jioni nikiambatana na rafiki zangu kibao,” Mbosso alilazimika kutangaza.

Awali alipotangaza Oktoba 28 kuwa ana jambo kubwa la kuzindua albamu yake fupi, ilipita siku chache baadae msanii Harmonize naye kutangaza tarehe hiyo hiyo kama siku ya kuachia albamu yake ambayo alisema haitokuwa na promotion yoyote ya kuiuza kwani kila kitu amekimalizia kwenye studio.

Washikadau katika sekta ya muziki wanahoji kwamba hii ni njia moja ya Harmonize kuendeleza vita vya ubabe na aliyekuwa baba wake katika muziki Diamond Platnumz, kwani msanii Mbosso anatokea lebo ya Diamond ambaye kwa sasa hawapikiki kwenye chungu kimoja na Harmonize.