Eric Omondi ampa changamoto Femi One kuenda Nigeria aone kama Tiwa atamtumbuizia

Omondi alichukizwa na kitendo cha msanii kutoka Nigeria kuja nchini na kutumbuiziwa na wasanii wa Kenya.

Muhtasari

• Alisema kwamba wasanii wa Kenya wanajiweka chini mno mpaka kuonewa huruma wakati wana nguvu za kuliteka soko la sanaa nchini mwao.

Omondi na staili mpya ya nywele
Omondi na staili mpya ya nywele
Image: Instagram

Mchekeshaji wa muda mrefu nchini Kenya, Eric Omondi ametoa changamoto kwa wasanii wa Kenya kujaribu kufanya ziara ya kimuziki nchini Nigeria ili pia wale wenzao kutoka taifa hilo kuwatumbuizia.

Omondi alikuwa akikejeli kitendo cha msanii Femi One wa Kenya kumtumbuizia Tiwa Savage wakati msanii huyo alikuwa nchini Kenya wikendi iliyopita kwa ajili ya kuzindua bidhaa mpya za vipodozi.

Alitupa makovu kwenye wasanii wa Kenya akisema kwamba iliwachukua wasanii zaidi ya 30 pamoja na kiingilio cha shilingi 500 pekee ili kujaza hafla ya kutumbuiza na kusema hilo hatolifumbia macho kamwe.

Alilinganisha hafla hiyo na kusema kwamba tukio sawa na hilo huchukua msanii mmoja tu kutoka Nigeria kujaza ukumbi hata kama kiingilio ni elfu 15.

“Ilichukua zaidi ya Wasanii 30 wa Kenya na Ksh 500 za kiingilio cha langoni ili kujaza tamasha la Kenya na unataka nipige makofi. Lazima muwe juu kwenye kitu marafiki zangu. Inachukua Mnigeria mmoja tu kujaza Tamasha na kiingilio cha getini ni hadi Ksh 15,000 na bado wanajazaa,” Omondi alisema.

Aliuliza ni kwa nini msanii Tiwa Savage akuje Kenya na kutumbuiziwa na wasanii wa Kenya na kutoa changamoto kwa wasanii wa Kenya pia kufanya udhubutu wa kuenda Nigeria waone kama watatumbuiziwa kule.

“Halafu kwanini Tiwa Savage Anazindua vipodozi nchini Kenya na Femi anamtumbuizia? Kwa nini haiwezi kuwa njia nyingine pande zote? Femi aende Lagos azindue vipodozi halafu Tiwa amtumbuizie. TAFAKARI MAKUBWA!!! AMKA!!! Sisi si wajinga!!!” Omondi alitema moto.