Zuchu ajibizana na shabiki aliyemsuta kwa kuiga uvaaji wa Diamond

Zuchu alimjibu kwa kumwambia kuwa hajui changamoto wasanii wanazozipitia katika kumbi za kimataifa kama Marekani.

Muhtasari

• Zuchu alisema kuwa watu wa nyumbani ndio adui wakubwa kwa wanamuziki wao na kuwataka kujifunza kuwakubali mwanzo.

Msanii Zuchu
Msanii Zuchu
Image: Instagram

Zuchu anaendelea kutangaza ziara yake ya kimuziki nchini Marekani licha ya shoo yake ya kwanza kubuma katika jimbo la Texas, Houston.

Jumanne jioni alipakia video kwenye ukurasa wake wa Instagram akiitangaza shoo yake ya Seattle itakayofanyika wikendi hii na kwenye kutoa maoni, mtumizi mmoja wa mitandao ya kijamii alimkaripia na Zuchu hakusita bali alijbu mipigo vikali.

Mtu huyo ambaye kutokana na jina lake ni mjasiriamali wa macheni na shanga alimsuta Zuchu vikali kuwa hajui kuvaa bali anaiga Diamond kwa uvaaji na hata kumtaka kuchukua funzo kutoka kwa mastaa wa kimataifa jinsi wanavyojibeba.

Jewelry World, kama aivyokuwa anajiita alimwambia Zuchu kujitahidi safari hii na kufanikisha shoo yake bure hivyo atajipata Analia kwikwi tena kama alivyolia wikendi iliyopita baada ya watu wachache kutokea kwenye shoo ya Houston.

“Natumai safari hii utaboresha gemu lako, zingatia sana katika wewe mwenyewe na wacheza densi wako. Hadhara itaelewa tu, hizi za kukata wimbo na kuita watu wasimame ni mambo ya bongo si ya huko. Halafu usivae kama Diamond, valia kitu kinachokutoa vizuri, kitu tofauti. Tafadhali angalia mastaa wa nje wanafanyaje shoo zao. Mubashara inamaanisha kuimba na kucheza mubashara, si kucheza densi tu,” shabiki huyo alimkoromea.

Zuchu alishikwa kulimeza hili na ikambidi kujikusanya kwa ujasiri wote na kulitema kwa jamaa huyo.

“Adui yetu mkubwa ni watu wetu wenyewe kwa sababu gani, Wallahi angevaa Rihamma ile nguo niliyovaa mngemvulia kofia na hata kuinunua wenyewe, angegonga vichwa vya habari. Unaona sasa ulivyokuwa hujui hata changamoto za Sanaa yetu kwenye kumbi kama zile. Hujui tunapewa masharti gani lakini hapa ulipo unaropokwa tu,” Zuchu alijibu.

Alisema kuwa watu ambao walikuwa wanamshangilia katika shoo ile iliyobuma ni wa kutoka nje wala si wa nyumbani Afrika Mashariki. Alimalizia kwa kuwataka mashujaa hao wa kutamba kweney intaneti kujifunza jinsi ya kuwapenda na kuwakubali watu wao mwanzo.