Zuchu, Rayvanny waiwakilisha Afrika Mashariki vyema kwenye tuzo za AFRIMMA

Wawili hao walishinda tuzo za Best Female na Best Male East Africa mtawalia.

Muhtasari

• Zuchu alimsifia bosi wake Diamond Platnumz na kumtaja kama shujaa wake ambaye muda wote na siku zote atasalia katika kumbukumbu ya moyo wake.

Zuchu na Rayvanny washinda tuzo za Afrimma
Zuchu na Rayvanny washinda tuzo za Afrimma
Image: Instagram

Wikendi iliyopita wasanii Zuchu na Rayvanny walipeperusha vyema bendera ya ukanda wa Afrika Mashariki katika tuzo za AFRIMMA zilizokuwa zikifanyika Marekani jimbo la Dallas.

Zuchu alishinda tuzo yake ya Afrimma kwa mara ya kwanza kabisa ambapo alikuwa anawania katika kitengo cha Best Female East Africa.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hizo, Zuchu aliwashukuru watu wa ukanda wa Afrika Mashariki wote waliomuaminia chini ya miaka miwili tu tangu atambulishwe rasmi kwenye Sanaa ya muziki wa Bongo Fleva na lebo ya WCB Wasafi.

Pia alimsifia bosi wake Diamond Platnumz na kumtaja kama shujaa wake ambaye muda wote na siku zote atasalia katika kumbukumbu ya moyo wake.

“Jana si yetu kupona kesho ni yetu kushinda 🏆ahsanteni sana kwa watu wangu wote wanakundi hii ni kwa wote. Mimi ni wa sasa na wa kesho,” Zuchu aliandika kwenye Instagram yake akifurahia kutuzwa.

 Kwa upande wake, Rayvanny ambaye ni mkurugenzi mkuu wa lebo ya Next Level Music alifurahia baada ya kushinda tuzo hiyo kwenye kitengo cha Best Male East Africa na kusema kwamba tuzo hiyo ni kwa wote waliomuaminia katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Rayvanny alisema kuwa katika maisha yake ameshinda tuzo nyingi lakini ile ya AFRIMMA ndio ilikuwa imekosekana na hivyo kuipata ni kama kumaliza mzunguko wa tuzo kwenye rafu yake.