Jamaa ataka kukutana na Elon Musk baada ya kujibu ujumbe wake Twitter

Kitema alisema hakuna lisiloshindikana chini ya jua na kuweka imani yake kuwa atakutana na tajiri huyo.

Muhtasari

• Musk mapema mwezi jana alijibu ujumbe wa jamaa huyo aliyesema kuwa Uganda wametuma setilaiti yao ya kwanza kwenda angani.

Jamaa ambaye tajiri Musk alijibu ujumbe wake
Jamaa ambaye tajiri Musk alijibu ujumbe wake
Image: Twitter

Lawrence kitema, mtumizi wa mtandao wa Twitter ambaye alijawa na furaha baada ya mmiliki wa mtandao wa Twitter, Elon Musk kujibu ujumbe wake sasa amesema lengo lake kubwa ni kukutana na mkwasi huyo namba moja duniani.

Kitema mapema mwezi jana aliandika kwenye Twitter akimtaarifu Musk kuwa taifa jirani la Uganda lilituma setilaiti yake ya kwanza kwenye angani mwaka huu huku akitaka kupata maoni ya Musk – ambaye kando na kumiliki Twitter, anamiliki kampuni ya magari ya umeme Tesla na pia kampuni ya kutuma setilaiti kwenda sayari zingine kwa jina SpaceX.

“Nchi yetu ya Afrika, Uganda ilituma setilaiti yake ya kwanza kwenda angani, hapo vipi Elon Musk?” aliandika.

“Hongera,” Musk alijibu.

Mwanaume huyo alichukua picha ya jibu hilo la Musk kwenye ujumbe wake na kupakia akijipiga kifua kuwa watu wamesema yeye ndiye mtu wa kwanza kutoka Afrika kupata jibu kutoka kwa Musk.

“Wakati Elon Musk anajibu tu tweets zako. Kuna mtu amesema mimi ni Mwafrika wa kwanza kupokea jibu la Elon Musk. (Kutoka kwa maoni sio mimi) 😂” Kitema alisema.

Sasa jamaa huyo ameibuka na kusema kuwa anataka kufuata mfano wa mchekeshaji Arap Uria aliyekutana na Peter Drury. Alisema naye anataka kukutana na Elon Musk uso kwa uso siku moja, huku akiweka Imani kuwa hakuna lisilowezekana chini ya jua.

“Ndoto zote zinawezekana, nataka kukutana na Elon Musk siku moja,” Kitema alsiema.

Alisema kuwa wengi huenda mkaona ni mzaha ila kwa upande wake ana Imani kuna mengi ambayo anataka kusemezana na Musk uso kwa uso kama atapata hiyo nafasi.