Diamond ataja ugonjwa wake, na ushauri wa daktari baada ya kugundulika na tatizo hilo sugu

Siku ya Krismasi mwaka uliopita, msanii huyo alilazwa hospitalini na kusema ndio siku yake ya Krismasi mbaya kabisa katika maisha yake.

Muhtasari

• Diamond alikanusha kuwa hakuwa anatafuta kiki kama ambavyo wengi walivyofikiria na kusema kuwa alikuwa anaugua kweli.

• Alizungumziwa kwa kina jinsi madaktari wake walimshauri ili kuepuka tatizo kama hilo kumtokea tena.

Msanii Platnumz akiwa hospitalini
Msanii Platnumz akiwa hospitalini
Image: INSTAGRAM

Msanii Diamond Platnumz kwa mara ya kwanza amefunguka kuhusu kilichomsababisha kulazwa hospitalini wiki moja iliyopita wakati dunia ilikuwa inasherehekea Krismasi.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha habari cha Wasafi, Diamond alisema kuwa ni kweli alikuwa mgonjwa, kinyume na dhana za wengi ambao walisema kuwa alikuwa anatafuta kiki kwa ajili ya wimbo wake mpya wa Chitaki.

Msanii huyo mchapakazi alifichua kuwa madaktari wake wamimshauri kupunguza kasi ya kufanya kazi na badala yake kuhakikisha kila siku anapata kulala angalau kwa saa 6 ili kuepuka kugonjeka tena.

Alisema ugonjwa wake ulikuwa ni kutokana na kuufanyisha mwili kazi kwa saa nyingi pasi na kupata pumziko la kutosha.

Msanii huyo alifichua kuwa katika siku nyingi mwishoni mwa mwaka jana, alikuwa anatumia muda mwingi sana kwenye studio kuandaa albamu yake mpya ambayo kwa bahati mbaya mwaka huo ulitamatika bila kuifanikisha kuiachia.

“Sikuwa nimepumzika. Nafanyia kazi albamu yangu ambayo ilitakiwa kuachiwa mwaka huu lakini haikuwezekana kwa sababu bado naifanyia kazi ili itakapotolewa ilete heshima kwa Tanzania. Ninamiliki karibu kampuni nne na nina wafanyikazi wengi kwa hivyo mambo yanapokuwa magumu kwenye kampuni, unapata mkazo na msongo wa mawazo na unaweza kuugua,” Simba alisema.

Msanii huyo alifunguka kuhusu ratiba yake ya kila siku ambayo ilikuwa inachukua muda mwingi sana na kumuachia muda mchache zaidi wa kupata kupumzika akili.

“Kila saa nne asubuhi ni lazima niwe ofisini kwa hiyo hiyo inamaanisha kuamka kabla ya saa 8:00 asubuhi. Nitakaa ofisini hadi saa 4:00 au 5:00 jioni kisha naelekea gym ambapo nafanya mazoezi hadi saa 7:00 au 8:00 usiku kisha naelekea studio. Kwa hivyo nimekuwa nikitumia muda mwingi huko wakati mwingine nikiondoka saa 6:00 asubuhi siku inayofuata kisha mzunguko unaendelea. Nilikuwa nimepumzika kwa muda mfupi sana.”