Bahati: Mimi na mke wangu tumeamua kuongeza mkataba wa mapenzi kwa mwaka mmoja

Wapenzi hao walikuwa kando ya ndege tayari kupaa kwa ziara ya likizo kujifurahisha mwaka unapoanza.

Muhtasari

• "Diana Marua na mimi tumeafikiana kuongeza mkataba wa mwaka mmoja katika mapenzi yetu,” Bahati

Bahati na Diana wakiwa tayari kupaa kwa likizo ya mwaka mpya
Bahati na Diana wakiwa tayari kupaa kwa likizo ya mwaka mpya
Image: Instagram

Msanii wa kizazi kipya nchini Bahati Kioko ambaye pia aliwahi jaribu bahati yake katika karata ya siasa amedokeza kuwa mwaka unapoanza, yeye na mkewe, Diana Marua wamefikia makubaliano ya kuongeza mkataba wa mwaka mmoja zaidi katika mapenzi yao.

Bahati kupitia ukurasa wake wa Instagram, alipakia picha wakiwa na mpenzi wake Diana Marua kando ya ndege wakiwa tayari kuliabiri kwa ajili ya kuzuru maeneo mazuri kujiburudisha.

“Tumeenda kufanya upya yamini zetu za ndoa. Diana Marua na mimi tumeafikiana kuongeza mkataba wa mwaka mmoja katika mapenzi yetu,” Bahati alisema huku akimla denda la kishua mpenzi huyo wake mama wa watoto watatu.

Bahati na mkewe Diana Marua wamekuwa si watu wa kufanya mambo yao faraghani kwani kila tukio dogo au kubwa katika maisha yao huwa hawachelewi kuwataarifu mashabiki wao.

Kwa upande wake, Marua alipakia picha akiwa ndani ya ndege hiyo pamoja na mwanawe wa kuasili Morgan Bahati na kusema kuwa walikuwa wanapaa kwenda sehemu nzuri ili kujiburudisha na kuanzisha mwaka mpya 2023 kwa kishindo cha aina yake.

Bahati amekuwa akishauriwa na wanoko wa mitandaoni kumuacha Marua, haswa kufuatia kipande cha video ambayo Marua alikuwa akimwaga mtama kwa kuku wengi kuhusu maisha yake ya awali kabla ya kukutana na Bahati.

Akisema ukweli wake bila woga, Marua alikiri kuwa aliwahi chumbiana na mwanaume aliyekuwa ameoa, huku pia akisema alichumbiana na wanaume wengi kwa wakati mmoja kama njia moja ya kukimu mahitaji yake ambayo yalikuwa mengi pasi na kuwa na mtu wa kuyakidhi.

Bahati alionesha sura yake ya kiume kwa kusema kuwa katu hawezi kumuacha Marua kwani hakumuoa kwa sababu ya watu bali kwa sababu zake binafsi – akitaja kuwa wale wanaomsema vibaya hawajui kuwa pengine tabia yake ya kuchumbiana na wanaume wengi ndio ilikuwa moja ya viungo vilivyomvutia kwake.