Bahati afichua kwa nini anaadhimisha siku ya kuzaliwa tarehe moja na mwanawe Morgan

Bahati alitimiza miaka 30 siku ya Alhamisi huku mwanawe akitimiza miaka 13.

Muhtasari

• Bahati alisema kuwa mwanawe Morgan Bahati  ni maalum sana kwake na anamweka karibu na moyo wake.

•Baada ya Bahati kutumbuiza, Morgan alikataa kurejea katika kituo hicho cha watoto na akataka kwenda naye.

Morgan Bahati na Bahati
Image: INSTAGRAM// BAHATI KENYA

Mwimbaji Kelvin Kioko almaarufu Bahati amefichua kuwa anashiriki tarehe sawa ya kuzaliwa na mtoto wake wa kulea Morgan Bahati.

Akizungumza siku moja baada ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, Bahati alisema kuwa mwanawe ni maalum kwake na anamweka karibu na moyo wake.

"Ninashiriki tarehe sawa ya kuzaliwa na mwanangu @morgan_bahati kwa sababu yeye ni maalum sana kwangu na ako karibu na moyo wangu❤," Bahati alisema kupitia kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili aliambatanisha ujumbe huo na picha yake na Morgan wakiwa wamevalia mavazi yanayofanana.

Bahati alitimiza umri wa miaka 30 siku ya Alhamisi  Desemba 22 huku mwanawe akisherehekea kutimiza miaka 13.

Mtunzi huyo wa wimbo 'Mama'  alimchukua Morgan kuwa mtoto wake mwaka wa 2014 wakati alipoenda kutumbuiza katika nyumba ya  watoto yatima ya ABC ambapo alikulia pia baada ya mama yake kuaga dunia.

Baada ya Bahati kutumbuiza, Morgan alikataa kurejea katika kituo hicho cha watoto na akataka kwenda naye.

Huku akizungumzia matukio ya kipindi hicho mwaka jana, msanii huyo alisema alikuwa wakati huo hakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha kumwezesha kuasili mtoto.

“Baada ya shoo mtoto  mdogoMorgan mwenye umri wa miaka 2 alilia kwenda na mimi nyumbani, ilikuwa ngumu kwangu kwa sababu nilikuwa bado natatizika kifedha.. Mbaya zaidi niliishi kwenye chumba kidogo na sikuwa na mtu wa kumlea mtoto kwa sababu nilkuwa nikiikaa peke yangu,'' alisema.

Morgan amekuwa akiishi na Bahati tangu wakati huo na mwimbaji huyo amekuwa akimtunza vizuri kama mtoto wake wa kuzaa.