"Ndiye mtu napenda" Morgan Bahati amtambulisha mpenzi wake kwa mamake Diana Marua

"Nampenda pia," Bi Angel alisema.

Muhtasari

•Diana alisema kuwa anajivunia mafanikio hayo makubwa ya mwanawe na akamhakikishia kuhusu upendo wake kwake.

•Morgan alifichua kuwa yeye na mpenziwe ni wanafunzi wenza ila wamekuwa wakisomea katika madarasa tofauti.

Diana Marua na mtoto wake wa kulea Morgan Bahati.
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Mwanavlogu mashuhuri Diana Marua alikuwa mama mwenye fahari baada ya mtoto wake wa kulea Morgan Bahati kuhitimu kutoka shule ya msingi hadi Sekondari ya Chini mnamo siku ya Jumamosi.

Huku akimsherehekea Morgan kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diana Marua alisema kuwa anajivunia mafanikio hayo makubwa ya mwanawe na akamhakikishia kuhusu upendo wake kwake.

"Ninajivunia kuitwa mama yako. Imekuwa ni safari na kukuona ukihitimu siku ya leo, nimeshangazwa na uaminifu wa Mungu. Nakupenda Morgan Bahati," Diana aliandika siku ya Jumapili.

Mama huyo wa watoto watatu alisema hayo baada ya kuhudhuria hafla ya kuhitimu kwa watahiniwa wa darasa la sita katika Juja Preparatory School  ambapo Morgan amekuwa akisomea.

Wakati wa hafla hiyo ya Jumamosi, Diana alipata nafasi ya kukutana na msichana ambaye anachumbiana  mwanawe. Morgan alimtambulisha mpenzi wake kwa mamake alipokuwa akiwapiga picha.

"Yeye ndiye mtu napenda," alisema Morgan.

Mpenziwe ambaye alionekana kuwa na haya alijitambulisha kama Angel na kukiri kuwa kwa kweli wanachumbiana.

"Nampenda pia," alisema.

Morgan alifichua kuwa yeye na mpenziwe ni wanafunzi wenza ila wamekuwa wakisomea katika madarasa tofauti.

Diana hakuwa na uhakika na cha kufanya ama kusema baada ya kukutana na mpenzi huyo wa mwanae lakini hakukosa kusifia uzuri wake.

"Sijui cha kusema, ni vizuri kukutana na wewe. Wewe ni mrembo!" alisema

Morgan alifichua kuwa kabla ya kukutana na Angel alikuwa kwenye mahusiano mengine kabla ya kusambaratika.

"Nilikuwa na mpenzi mwingine tukatenga, nitakuonyesha," alimwambia mama yake.

Baada ya kushuhudia hayo, Diana kwa mshangao mkubwa alisema, "Katika darasa la sita mimi sikujua chochote."

Rapa huyo alibainisha kuwa anajivunia hatua ya mwanawe ila akamshauri azingatie masomo yake kwanza.

"Ninajivunia wewe. Najua kuhusu mambo ya mpenzi lakini cha muhimu ni masomo. Nataka upate alama nzuri na usikilize walimu wako. Mengine yatakuja," alimwambia.

Morgan alijigamba kuhusu ubabe wake wa kuvutia wasichana ila akamhakikishia mama yake kwamba mahusiano hayataadhiri masomo yake.

"Tunafanya vizuri shuleni, mbona tusifanye hivyo," alisema.