Ujumbe wa Anjella akiiaga rasmi lebo ya Harmonize, Konde Music Worldwide

Mwezi Novemba mwaka jana, Harmonize alitangaza kutamatisha mkataba wa Anjella katika lebo hiyo akipuuza uvumi kuwa anamdai.

Muhtasari

• Kuaga rasmi kwa Anjella kunaashiria kuwa wameyamaliza yale yaliyokuwa yakikwamiza kuondoka kwake ikiwemo kupata hakimiliki za kazi zake za muziki.

Anjella aaga rasmi Konde Gang
Anjella aaga rasmi Konde Gang
Image: Instagram

Msanii w kike wa kizazi kipya nchini Tanzania Anjella baada ya kimya cha muda mrefu kuhusu mustakabali wake, hatimaye ametoa tamko lake kuhusu kuondoka kwake katika lebo ya Konde Music Worldwide.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Anjella ametoa tamko la kuaga mashabiki na wafuasi wa lebo hiyo inayomilikiwa na msanii Harmonize na kutoa shukrani kwa kushikwa mkono katika kipindi kile ambacho alipata kufanya kazi chini yao.

“Kwaheri Konde Gang na ahsante,” Anjella aliandika kwenye picha ya nembo ya lebo ya Konde Music Worldwide.

Tamko lake rasmi linadhibitisha kuwa msanii huyo amesuluhisha kila kitu katika mgogoro wa ndani uliohusisha kutamatishwa kwa mkataba wake pamoja na hakimiliki za akaunti zake za mitandao ya kijamii pamoja na nyimbo ambazo alirekodi akiwa chini ya lebo ya Harmonize kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, Harmonize alidhibitisha kuwa mkataba wa Anjella katika lebo hiyo ulikuwa umetamatishwa na kukanusha madai kuwa walikuwa wameshikilia akaunti zake pamoja na hakimiliki za kazi za muziki.

Harmonize alitoa wito kwa yeyote ambaye alikuwa anataka kuendelea kumsaidia Anjella kufanay hivyo kwani yeye alikuwa msanii huru tangia pale.

“Nilikutana na Anjella akiwa amejikatia tamaa akiwa na ndoto kichwani. Sikujiangali nina kiasi gani, nilijiamini kwa kuwa wapo watu wanaonisapoti bila kuwalipa senti tano basi watasapoti kipaji cha dada Anjella. Kama kunaye anayeweza kumwendelezea kipaji chake ni faraja kwangu, asisite kujitokeza. Puuza siasa za kusema sijui namdai mahela, sijawahi kumtoza hata senti moja,” Harmonize alisisitiza.

Taarifa ya Anjella kuaga kwa njia ya heshima imesifiwa pakubwa na watu ambao wamesema ametumia busara kubwa kuaga kwa namna hiyo pasi na kuzungumza maneno mengi ambayo pengine yangeibua ukakasi mbeleni.