Harmonize athibitisha Anjella kuondoka Konde Gang, akanusha kudai

Msanii huyo alikanusha madai yanayosambazwa mitandaoni kwamba anamdai Anjella mamilioni ili kuvunja mkataba wake.

Muhtasari

• Alisema kuwa kama yupo mtu yeyote mwenye uwezo wa kumsaidia Anjella kuendeleza kipaji chake basi asisite kujitokeza.

Harmonize adhibitisha kuachana na Anjella
Harmonize adhibitisha kuachana na Anjella
Image: YouTube screengrab

Mkurugenzi mkuu wa rekodi lebo ya Konde Music, Rajab Abdul ‘Harmonize’ leo Jumamosi Novemba 5, 2022 amethibitisha taarifa za kuachana na msanii wake Angelina Samson ‘Anjella’

Kupitia Instagram yake, Harmonize ameweka wazi kuhusu hayo na kuwachimba mikwara wale wote wanaomsema kwamba anamdai Anjella kiasi cha mamilioni ya pesa ili kumuachilia kuondoka kwenye lebo hiyo.

Msanii Harmonize amechukua fursa hiyo kuhadithia kiasi jinsi alivyokutana na msanii Anjella na kumshika mkono mpaka kukipaisha kipaji chake pasi na kumtoza hata senti.

Alisikitishwa jinsi watu wanamsema kuwa anamkandia Anjella kwa kushikilia mitandao yake ya kijamii pamoja na baadhi ya kazi zake mpaka pale atakapolipa. Harmonize amekanusha madai hayo na kusema kwamba hamdai Anjella hata sillingi.

Alimaliza kuwaomba wenye hisani na ambao wako tayari kutoa msaada wao kwa Anjella kufanya hivyo ili kumwezesha kutimiza ndoto zake kimuziki.

“Nilikutana na Anjella akiwa amejikatia tamaa akiwa na ndoto kichwani. Sikujiangali nina kiasi gani, nilijiamini kwa kuwa wapo watu wanaonisapoti bila kuwalipa senti tano basi watasapoti kipaji cha dada Anjella. Nulichoangalia ni ndoto na hasa za mtoto wa kike. Nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu, najua kuna wenye uwezo mkubwa kunizidi, ukizingatia nimeanza juzi,” Harmonzie alisema.

“Kama kunaye anayeweza kumwendelezea kipaji chake ni faraja kwangu, asisite kujitokeza. Puuza siasa za kusema sijui namdai mahela, sijawahi kumtoza hata senti moja,” Harmonize alisisitiza.

Angela alitambulishwa kwenye lebo hiyo Machi 11, 2021 ambapo aliachia wimbo ‘Kama’ aliomshirikisha Harmonize na mpaka sasa wimbo huo umeshatazamwa zaidi ya mara milioni tatu kwenye mtandao wa Youtube.