'Panga watu wako,'DP Gachagua amuonya Samidoh kufuatia kisanga cha Dubai

Nyamu alibainisha kuwa hakuwa na majuto yoyote kufuatia kile kilichotokea Dubai, na kuahidi kuwa tukio hilo lilikuwa la mwisho.

Muhtasari
  • Gachagua alikuwa akirejelea kisa cha hivi majuzi ambapo Seneta Mteule Karen Nyamu alinaswa kwenye video akipigana na mke wa Samidoh

Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa amemtaka mwimbaji maarufu wa Mugithi Samidoh kushughulikia masuala yake ya ndoa la sivyo ataadhibiwa.

Akisisitiza kwamba mwimbaji huyo ambaye pia ni afisa wa polisi anawaangusha mashabiki wake, Bw Gachagua alimweleza Samidoh, jina halisi la Samuel Muchoki, kwamba yeye ni aibu kwa kuruhusu masuala yake ya faragha kumwagika hadharani.

"Wewe sasa Samidoh unajua tunakupenda lakini kuna mahali unatuangusha kidogo. Samidoh, u control hii watu wako... Hakuna ndovu hushindwa na pembe zake..." alisema.

Gachagua alikuwa akirejelea kisa cha hivi majuzi ambapo Seneta Mteule Karen Nyamu alinaswa kwenye video akipigana na mke wa Samidoh katika klabu moja huko Dubai mbele ya Samidoh.

Alikuwa akizungumza huko Gatundu wakati wa mazishi ya dadake Waziri wa Biashara Moses Kuria.

Haya yanajiri takriban mwezi mmoja baada ya Karen Nyamu kukatiza uhusiano na mpenzi wake wa muda mrefu na Samidoh.

Karen alitangaza mwisho wa uhusiano wake na baba huyo wa watoto wake wawili katikati mwa Desemba kufuatia tukio la ugomvi uliowahusisha wao na mke wa Samidoh Edday Nderitu katika eneo moja la burudani jijini Dubai.

Nyamu alibainisha kuwa hakuwa na majuto yoyote kufuatia  kile kilichotokea Dubai, na kuahidi kuwa tukio hilo lilikuwa la mwisho.