Xtian Dela: Ninapambana na matatizo ya wasiwasi, siamini katika Ukristo tena!

Dela alisema kuwa haamini katika Ukristo tena kwani mbinguni na kuzimuni vyote vimo humu humu tu duniani.

Muhtasari

• Mwanablogu huyo alifichua kwamba kwa wakati mmoja aliwahi jaribu kujitoa uhai kutokana na msongo wa mawazo.

• Mama yake alisema Dela aliwablock wanafamilia wote bila kutaka kuonana na hata mmoja kwa miaka 4 sasa.

Mwanablogu Xtian Dela
Mwanablogu Xtian Dela
Image: Facebook

Mwanablogu Xtian Dela amefunguka kuwa anapitia matatizo ya wasiwasi kwa sasa hivi, siku chache baada ya mama yake kufunguka kuwa kwa miaka mine iliyopita, hajawahi kuonana na mwanaye huyo.

Zogo lilianza baada ya mama yake Dela ambaye pia ni mwigizaji Naomi Nyongesa kufanya mahojiano na mwanablogu mmoja akilia kwa uchungu kwamba hajaonana na mwanawe.

Nyongesa alisema kwamba Dela alimblock kwenye mitandao yote ya kijamii, huku akimtupia lawama mpenzi wa Dela, mwanamitindo Fatma Banj kwa kumbadilisha mwanawe kiasi cha kwamba hataki tena kuonana wala kuongea na mtu yeyote kutoka ukoo wake.

Dela kupitia ukurasa wake wa Twitter alasiri ya Jumanne, alishiriki kwamba hayuko sawa bali anapambana na tatizo kubwa la wasiwasi.

Pia alishiriki tovuti moja inayoelezea aina mbalimbali za matatizo ya wasiwasi ambayo watu wengi huchukulia kawaida bila kujua athari zake.

“Kwa sasa, mimi binafsi NINAPIGANA na Matatizo ya Wasiwasi. Jifunze ZAIDI kuhusu Aina TOFAUTI za Ugonjwa huu wa Akili,” Xtian Dela alisema.

Awali baada ya video ya kitambo ya mwanablogu huyo akiimba wimbo wa injili na mama yake ilisambazwa mitandaoni. Dela alionekana akicheza na gitaa kwa madaha huku akiimba kiitikio cha wimbo huo kwa sauti nzuri, lakini mwenyewe aliweka wazi kwamba haamini tena katika dini ya Ukristo wala dini yoyote duniani.

“Mimi si Mkristo tena; kujua ukweli; mbingu na kuzimu vyote viko hapa. Sisi tuko karma,” Dela alisema katika video moja kwenye mtandao wa YouTube akidokeza kwamba kuna kitu kibaya sana kilichompiga dafrau hadi kwenye shimo la giza.

Xtian ambaye amekuwa kimya kwa mwaka mzima pia alilalamika kwamba kila kitu alichogusa kilishuka. Pia alisema kwamba alijaribu kujiua.

Mwanablogu huyo pia alisimulia kwa uchungu wakati alipotajwa kuwa tapeli ambaye aliwaibia watu na kuwashutumu watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwa watu wa kumsimanga mtu bila huruma.