Bila zawadi hakuna kuingia kwa harusi yangu - Akothee

Hii itakuwa harusi ya pili kwa mjasiriamali huyo tajiri zaidi kutoka nchini Kenya.

Muhtasari

• Mwishoni mwa wiki jana, msanii huyo aliagiza shela la harusi, ghali kutoka mataifa ya kigeni na alipakia video akionekana kuishusha kutoka kwa ndege.

Akothee atoa mashariki kwa harusi yake.
Akothee atoa mashariki kwa harusi yake.
Image: Facebook

Msanii na mjasiriamali namba moja kutoka nchini Kenya, Esther Akoth almaarufu Akothee anaendelea kujiandaa vilivyo kwa harusi yake kubwa ambayo itafanyika siku tano zijazo na mpenzi wake mzungu alimbatiza jina Mr Omosh.

Msanii huyo sasa ametangaza kwamba katika harusi yake, kiiingilio ni zawadi, na kama utakuwa hauna zawadi basi milango ya harusi yake utaioneka kwa umbali tu wala hutoruhusiwa hata kukaribia, achia mbali kuingia.

Aliwataadharisha wafuasi wake kuwa ni vizuri amenyoosha maelezo yake  mapema ili wasije kuanza kumlaumu kwamba hakuwaambia ili wajipange, kwani wako na takribani wiki moja kujihami na zawadi kama kweli wanataka kushuhudia harusi hiyo ambayo ameitaja kuwa ya kihistoria.

“Jua tuu bila zawadi huingii. Nimesema mapema Ndio bora 🤣🤣🤣🤣. Mambo ya Ooh sikujua hata nilete nini Hakuna wakati huu,” Akothee alisema.

Mwishoni mwa wiki jana, msanii huyo aliagiza shela la harusi, ghali kutoka mataifa ya kigeni na alipakia video akionekana kuishusha kutoka kwa ndege.

Msanii huyo alisema kwamba ainunua gauni hilo la harusi kwa takribani laki saba, akisema kwamba yuko radhi kuzikwa kwa hilo gauni endapo atafariki.

Hii iakuwa harusi yake ya pili, baada ya kufanya harusi ya kwanza akiwa na umri mchanga, harusi ambayo amekuwa akiitaja kama iliyompa mafunzo makubwa, ya kiwango duni na ambayo hata hivyo haikudumu kwa muda mrefu.