Elon Musk atangaza tarehe ya mwisho kuondolewa beji za bluu kwa akaunti hazijalipa

Nchini Kenya tayari akaunti ya naibu rais Rigathi Gachagua imenyanganywa utambulisho huo wa beji ya bluu.

Muhtasari

• Musk alitangaza kuwa akaunti zenye utambulisho wa beji za bluu wangehitaji kulipia dola 8 kila mwezi ili kuzihifadhi.

• Hata hivyo, hatua hiyo imepokea pingamizi kali kutoka kwa watu mashuhuri ambao wameapa kutotii agizo la mmiliki wa Twitter.

Musk atangaza tarehe ya mwisho kuondolewa kwa beji za bluu.
Musk atangaza tarehe ya mwisho kuondolewa kwa beji za bluu.
Image: Twitter

Tajiri namba mbili duniani na mmiliki wa Twitter Elon Musk ametangaza tarehe ya mwisho ya kuondolewa kabisa kwa beji za bluu kwenye akaunti zote za Twitter ambazo wamiliki wao hawatakuwa wamelipia kiasi cha kila dola nane kila mwezi ili kuzihifadhi beji hizo.

Musk ambaye ni mtu wa kutweet sana kwenye mtandao huo wake awali alikuwa ameseka kuwa kuanzia Aprili mosi, akaunti zote zenye beji za bluu na ambazo hazijalipia gharama ya beji hizo zingenyanganywa utambulisho huo.

Lakini kufikia Aprili mosi, hakuna kubwa lililoshuhudiwa kwani watu wengi tu wenye beji za bluu na ambao hawajalipia badi wanaona utambulisho wao, isipokuwa baadhi ya taasisi na watu wachache tu ambao walikuwa wa kwanza kupatwa na msumemo wa amri ya Musk.

Tayari ukurasa wa jarida la New York Times ulikuwa wa kwanza kunyanganywa beji hiyo ukifuatiwa na akaunti ya naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua na pia juzi msanii Doja Cat alitangaza beji ya utambulisho wake kuondolewa.

Kufuatia ukimya huo kuwa wengi bado wanaendelea kuwa na beji hizo pasi na kulipia, Musk amefoka kwa mara nyingine akisema kuwa ifikapo Aprili 20, hakuna akaunti itakuwa na utambulisho wa beji ya bluu bila kuilipia.

“Tarehe ya mwisho kabisa ya k uondolewa kwa beji za utambulisho za bluu kwenye akaunti za Twitter ni Aprili 20,” Musk alitweet.

Musk mapema mwaka huu alitangaza kuwa akaunti za Twitter zinazotaka kuendelea kuhifadhi nembo hiyo ya utambulisho wa bluu zitalazimika kuzama mfukoni na kulipia gharama ya shilingi elfu moja na ushee, sawa na dola 8 za Kimarekani kila mwezi.

Hata hivyo, hatua hiyo imepata pingamizi kali kutoka kwa baadhi ya watu mashuhuri ambao wamepinga vikali hatua ya Musk kutaka beji hizo kulipiwa wakati awali zilikuwa zinatolewa bure ili kulinda na kutofautisha watu hawa kutoka kwa watu ghushi amabo wangetumia majina yao kuwalaghai watu.

Baadhi ya watu maarufu ambao wamesema hawako tayari kulipia gharama hiyo ni pamoja na mwanahabari wa CNN kutoka Kenya Larry Madowo, mchezaji wa mpira wa vikapu James LleBron miongoni mwa wengine.