'Maadui' Harmonize na Diamond wakutana uso kwa uso kwenye futari ya Ramadani

Diamond na harmonize hawaonani jicho kwa jicho tangu ugomvi wa 2019 lakini safari hii walikutana kwa ajili ya chakula cha Ramadani.

Muhtasari

• Futari ni mojawapo ya chakula cha kidini ambacho huliwa wakati wa Ramadani na mara nyingi hufanyika na jamii, yaani watu wanakusanyika ili kufuturu pamoja.

Harmonize wakutana uso kwa uso kwenye futari
Harmonize wakutana uso kwa uso kwenye futari
Image: Screengrab//YouTube-SNS

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019, wasanii Harmonize na aliyekuwa baba yake katika Sanaa ya muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz wamekutana uso kwa uso kwenye chakula cha kufuturu jioni ya Jumamosi ya Aprili 15.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania aliandaa futari kubwa Jumamosi katika ikulu ya Dar es Salaam na kuwaalika watu mbali mbali wakiwemo viongozi wa serikali na wasanii wa miziki pamoja pia na waigizaji.

Sasa baada ya futari hiyo ya Ramadani kukamilika vizuri Jumamosi jioni, gumzo la mitandaoni ni baada ya wasanii hao wawili wanaodhaniwa kuwa maadui wasioweza kuonana jicho kwa jicho, kukutana kwenye futari hiyo.

Futari ni mojawapo ya chakula cha kidini ambacho huliwa wakati wa Ramadani na mara nyingi hufanyika na jamii, yaani watu wanakusanyika ili kufuturu pamoja.

Katika picha ambazo zinaenezwa mitandaoni kutoka kwa mkusanyiko huo, picha na ambazo hakuna mmoja kati ya wasanii hao ameichapisha kwenye kurasa zake, zinawaonesha wakiwa wameketi pamoja kwa kukaribiana kabisa kiasi kwamba kila mmoja anaweza kumuona mwenzake.

Harmonize ameketi kwenye safu ya mbele akiwa na meneja wake huku Diamond akiwa ameketi nyuma pembezoni kidogo kando na muigizaji Steve Nyerere, sehemu ambayo kwamba Harmonize akigeuka nyuma kidogo tu upande wa kushoto moja kwa moja macho yake yanatua kwenye kilemba cha Diamond.

Hii ndio mara ya kwanza walionekana wamekaribiana angalau kidogo, kinyume na siku ya mazishi ya hayati rais Magufuli ambapo waliketi mbali kidogo kutoka kwa mwingine.

Wasanii haoc ambao walikuwa marafiki wakubwa, Diamond akiwa kama bosi wa Harmonize walikinukisha mwishoni mwa mwaka 2019 baada ya Harmonize kujitema nje ya WCB Wasafi, lebo iliyomkuza na kumlea akidai kuwa alikuwa anadhulumiwa na kunyanyaswa kimapato ya muziki.

Baada ya kuondoka kwa kuvunja mkataba wake kishari, ambapo alidai kulipa milioni 600 za Kitanzania, alienda zake na kuanzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide na kuanzisha mfululizo wa mashambulizi dhidi ya bosi wa zamani akimyuhumu kwa mambo mbali mbali.