Alikiba aomba radhi kwa kuimbia mayatima wimbo wa 'Utu' wakati wa Ramadani

Kwa Waislam, wakati wa Ramadani mja hafai kujishughulisha na mambo ya kidunia ikiwemo kushiriki ngono wakati wa saumu (wakati wote baina ya alfajiri na magharibi).

Muhtasari

• Alikiba alijitetea akisema kuwa hadhani Mungu atamhukumu kwa sababu alikuwa anawafurahisha mayatima tu.

• Kwa Taratibu za Ramadani, Muislamu hafai kufanya mambo yanayotajwa kuwa ya kidunia katika kipoindi hicho kitakatifu.

Alikiba aomba rashi kuimba wimbo wa kidunia wakati wa ramadani.
Alikiba aomba rashi kuimba wimbo wa kidunia wakati wa ramadani.
Image: Screengrab//RickMedia

Msanii Alikiba ameomba radhi kwa jamii ya Waislamu baada ya kutumbuiza katika futari na watoto mayatima kwa wimbo wake wa Utu.

Msanii huyo alisema kuwa haikuwa nia yake kuimba wimbo huo ikizingatiwa kwamba huu ni mwezi mtukufu wa Ramadani, lakini alitaka kufanya hvyo ili kuwaridhisha watoto hao ambao ndio walimuomba awatumbuize na kibao chenyewe.

Kulingana na tamaduni za dini ya Kiislamu, mwezi wa Ramadani ni mwezi mtukufu ambao kila mja anapaswa kujiweka safi pasi na kujipata katika njia ya mambo ya kidunia, na hivyo sehemu ya waislamu kindakindaki huenda walikwasika kwa namna Fulani kumuona Alikiba akiimba wimbo wa kidunia wakati wa mwezi mtukufu.

Kiba akijibu kuhusu swali hilo kutoka kwa mwanahabari, alianza kwa kukiri kwanza alikosea lakini kujitetea kuwa Mungu atamsamehe kwani alitaka kuwafurahisha mayatima tu.

“Kiukweli mwenyezi Mungu huwa anawasamehe waja wake wakiwa wamekosea, lakini nilikuwa sina mawazo hayo, lengo lilikuwa ni kuwafurahisha mayatima kwa sababu waliniomba niwaimbie kidogo. Na walitaja wimbo ambao walitaka niwaimbie. Nadhani mwenyezi Mungu hatanihukumu kwa hilo kama ataona nimefanya busara kuwafurahisha mayatima,” Alikiba alisema.

Alisisitiza kwamba lengo halikuwa hilo kwani yeye amekulia kwenye jamii ya Kiislamu na anaelewa fika mambo ambayo mja anafaa kujitenga nayo wakati wa mfungo wa Ramadani.

“Lengo lilikuwa si kuyaingiza mambo haya ambayo tunayafanya katika mwezi huu wa kufanya ibada haswa katika mfungo wa Ramadani,” Alikiba alisema.

Kando na kutotakiwa kuimba miziki ya kidunia wakati wa Ramadani pia, kuna maswala mengine mengi ambayo Wailsamu hawafai kufanya katika mwezi mtukufu wa Ramadani.

Tendo kubwa ambalo linaonekana moja kwa moja kufanywa na waislamu katika kipindi hiki cha mfungo ni kujizuia kunywa na kula kutoka alfajiri (kuchomoza kwa jua) mpaka magharibi (kuzama kwa jua).

Haijalishi, mtu awe masikini ama tajiri, awe na chakula ndani ama asiwenacho, madhali wanakiri kwa yakini kuwa ni waislamu basi hujizuia kula na kunywa.

Kwa wanandoa, tendo la kujamiiana halitakiwi kufanyika wakati wakiwa ndani ya saumu (wakati wote baina ya alfajiri na magharibi). Endapo watafanya hivyo ndani ya muda wa kufunga basi funga yao itakuwa imebatilika.