Ronaldo afutilia mbali uvumi wa kuachana na mkewe Georgina, "Mapenzi bado yapo!"

Awali kulikuwa na uvumi utoka Ureno kuwa uhusiano wa Georgina Rodriguez na mamake Ronaldo haukuwa sawa na mama mtu alikuwa anamtaka mwanawe kumtema mkewe.

Muhtasari

• Picha hiyo ilionekana kuosha kabisa uvumi huo wote ambao ulikuwa unadai kwamba Georgina hana raha na mamake Ronaldo na muda mwingi hukaa kwenye duka lake huko Saudia.

Ronaldo na Mkewe katika hafla ya siku yake ya kuzaliwa
Image: Christiano Ronaldo (Facebook)

Staa wa soka kutoka Ureno Christiano Ronaldo ameibuka na kufutilia mbali uvumi ulioibuliwa na wanahabari wa michezo nchini Ureno kwamba uhusiano wa mkewe Georgina Rodriguez na mamake Ronaldo umezorota.

Uvumi huo uliibuka katika kipindi cha mazungumzo cha kituo cha runinga cha CMTV cha Ureno Noite das Estrelas, ambapo mwandishi wa habari Quintino Aires, rafiki wa karibu wa mama wa Ronaldo, alidai kuwa tabia za mwanasoka huyo zilionyesha kwamba hakuwa na furaha katika maisha yake ya kibinafsi.

"Haishi wakati wa furaha, na kadiri anavyosonga mbali na mama yake, ndivyo anavyopungua. Na sote tunajua kwa nini anazidi kuwa mbali na familia yake,” Aires alisema, akimnyooshea kidole mpenzi wa Ronaldo, Georgina Rodriguez.

Lakini Ronaldo ambaye hajawahi kulizingumzia hilo alifutilia mbali madai hayo kwa picha ya pamoja wakipigana mabusu na mkewe huku wakigonga cheers ya glasi za juisi na kuweka maneno mawili;

“Cheers kwa mapenzi!”

Picha hiyo ilionekana kuosha kabisa uvumi huo wote ambao ulikuwa unadai kwamba Georgina hana raha na mamake Ronaldo na muda mwingi hukaa kwenye duka lake huko Saudia.

"Georgina hutumia siku yake katika duka la jumla huko Riyadh, na hiyo ndiyo sababu mojawapo kwa nini Cristiano hafurahishwi na hadithi hii," aliongeza mwanahabari huyo aliyekuja na uvumi huo.

Ronaldo na mkewe walikutana mwaka 2016 ambapo wamekuwa wakiishi pamoja kama wanandoa licha ya kutofunga harusi halali.

Mapema mwaka huu, Ronaldo na Georgina waliweka rekodi ya kuwa watu wa kwanza kuruhusiwa kuishi nchini Saudi Arabia bila kuoana rasmi, kwani sheria za Kiislamu katika taifa hilo zinasema kwamba hakuna watu wanaoruhusiwa kuishi kama wanandoa pasi na kuoana rasmi.