Diamond: Rafiki wangu wa kike alienda kwa mganga kuniroga ili nimuoe, nimpe gari

Diamond alisema alipokea voice note 3 ambapo huyo mwanadada alikuwa anazungumza na mganga akitaka kumroga yeye, mamake na ndugu zake.

Muhtasari

• "Nikamfuata nikamwambia huyu ni wewe, kwa nini unaenda kwa mganga unataka uniroge mimi, umroge mamangu kwa sababu gani" - Diamond alisema.

Diamond asema rafiki wake wa kike alitaka kumroga ili amuoe.
Diamond asema rafiki wake wa kike alitaka kumroga ili amuoe.
Image: Instagram

Video ya msanii wa kizazi kipya Diamond Platnumz akisimulia jinsi rafiki wake wa kike alivyomwendea kwa mganga ili kumfanya zamwamwa ilmradi ampe nyumba pamoja na kumuoa imeibua hisia mseto mitandaoni.

Katika video hiyo ambayo kiuhalisia si ya kitambao vile, Diamond Platnumz japo alidinda kumtaja mwanamke huyo alifichua ukweli kwamba alitumiwa sauti yake jinsi alienda kwa mganga kumfanyia ulozi.

“Kuna moja ya mtu, sitaki kumtaja jina lake, ni mwanamke ambaye alikuwa ameenda kwa mganga, akaongea naye sijui aniroge mimi sijui nimuoe, sijui nimpe nyumbe na vitu vingine vingi vingi,” Diamond alisema.

Diamond alisema kuwa wala haongopei kwani ni kitu ambacho kilitokea na alitumiwa sauti na kabisa alihakiki ni yeye huyo mwanadada.

Baada ya kusikia hivyo, Diamond alisema kuwa alimfuata mwanadada huyo na kumtumbulia jipu moja kwa moja usoni akitaka kujua kwa nini alitaka kufanya uamuzi huo wa ajabu.

“Ni kitu kipo, voice note zinatambaa na mimi nilitumiwa halafu unajua nasikia kitu ambacho najua huyu ni yeye. Nikamfuata nikamwambia huyu ni wewe, kwa nini unaenda kwa mganga unataka uniroge mimi, umroge mamangu kwa sababu gani, kwa nini ufanye vitu kama hivyo, haina maana!” Diamond alifunguka mfululizo wa maswali aliyomtiririkia mwanadada huyo.

Msanii huyo alisema kwamba voice note hizo alitumiwa tatu na zilivyomfikia zilimkata maini vibaya sana, akajisikia vibaya sana kwani huyo hakuwa anataka kumroga yeye tu bali pia mama yake lakini pia na baadhi ya ndugu zake.