Nilifukuzwa shule tano kwa sababu ya ukaidi wangu na kutopenda shule - Fantana

Licha ya kukataliwa na zaidi ya shule nne, Fantana sasa ni mrembo mkwasi ambaye atakuwa katika filamu ya Netflix ya Young, Famous & African msimu wa pili itakayooneshwa Mei 19.

Muhtasari

• Fantana alisema kuwa mama yake hakuwahi kumlazimisha kwenda shule kwa sababu alikuwa anajua kuwa yeye si mtu wa masomo.

• Licha ya kutopenda masomo, Fantana aliinuka hadi kujizolea umaarufu na utajiri wa kumwezesha kushiriki kwenye filamu ya Netflix - Young, Famous & African.

Fantana, msanii wa Ghana ambaye atakuwepo kwenye Young, Famous & African ya Netflix.
Fantana, msanii wa Ghana ambaye atakuwepo kwenye Young, Famous & African ya Netflix.
Image: Instagram

Mwanamuziki aliyefeli wa nchini Ghana, Fantana amefichua jinsi hali yake ya kutopenda shule ilivyomuingiza kwenye matatizo makubwa.

Akizungumza katika mahojiano na mtangazaji mmoja wa nchini humo, Fantana alifichua jinsi alivyokuwa akienda shule kila mara na jinsi alivyokuwa mwanafunzi mbaya.

Msanii huyo ambaye sasa ni mwanasosholaiti mkubwa aliyejitengenezea jina na kujizolea nafasi ya kuonekana kwenye mfululilzo wa kihalisia wa Netflix alikiri bayana kuwa hakuwa anapenda maisha ya shule kabisa katika utoto wake.

“Sikuwahi kupenda kusoma hivyo wakati wowote nikienda shule nilifanya mambo mabaya makusudi ili nifukuzwe. Nilibadilisha shule mara tano hivi na nikafukuzwa shule zote. Nilichukia shule…niliwachukia walimu…nilichukia tu dhana ya kukaa chini na kusikiliza mihadhara ya kuchosha,” Fantana alifichua.

Aliendelea na kuongeza kuwa mamake ambaye ni mbunge nchini Ghana hakuwahi kumsumbua wakati alikataa kwenda shule kwa sababu alijua yeye(Fantana) anachukia shule.

“Mama yangu alikuwa mzuri lakini hakuwahi kunilazimisha kwenda shule. Sikuishi naye Marekani lakini alikuwa huko kila wakati. Nina dada ambaye ana kipaji zaidi yangu. Dada yangu anapenda shule na anapenda kusoma kwa hivyo yeye ndiye mwenye akili Zaidi,” Fantana aliongeza.

Fantana ambaye ni binamu wa mwigizaji nyota wa dancehall Shatta Wale pia alifichua kuwa aliamua kukimbilia Ghana alipochoka shule na mihadhara ya kuchosha huko Marekani.

Lakini Fantana alihakikisha amehitimu kutoka Shule ya Upili ili kuwathibitishia kanisa lake na Waghana kwamba hakuwa bubu.

Kwa sasa, mwanasosholaiti huyo mwenye ushawishi mkubwa amehakikisha kwamba licha ya ndoto yake ya kuwa mwanamuziki kutofana sana, bado anaweza jinafasi katika mambo mengine.

Wiki tatu zilizopita Netflix walitangaza mfululizo wa kihalisia ambao utakuja sehemu ya pili kwa jina Young, Famous & African – mwendelezo unaoangazia maisha ya vijana wa Kiafrika ambao wana utajiri mkubwa na umaarufu pia.

Fantana ni mmoja wa wale ambao watakuwa katika filamu hiyo ambayo sehemu ya pili inashuka mnamo Mei 19 kwenye jukwaa la Netflix.

 Hii inaonesha ni jinsi gani aliweza kufaulu licha ya kutopenda shule na pia muziki wake kutofaulu sana.