Msingemuona Mbosso Wasafi kama sio talanta yangu - Enock Bella, msanii mwenza Yamoto Band

Enock alisema kuwa kuna kipindi amevizia uongozi wa Wasafi na kukaa karibu nao hata kufanya kazi nao akitarajia wangemchukua lakini hakuweza kufanikiwa na hivyo kuondoka.

Muhtasari

• "Mimi nilikuwa naona jitihada zangu ambazo nilikuwa nazifanya kwa Wasafi sana, lakini mbona kuna kitu nakikosa? " - Enock Bella.

Enock Bella asema bila yeye Mbosso asingekuwa Wasafi
Enock Bella asema bila yeye Mbosso asingekuwa Wasafi
Image: Instagram

Miaka kadhaa baada ya bendi asili ya Yamoto kusambaratika na kila mmoja kwenda zake, wasanii hao wote wanazidi kutoonyesha ushirikiano kama ambavyo walivyokuwa na ukaribu enzi zile wakiwa chini ya mwavuli wake.

Yamoto Band ilikuwa inajumuisha wasanii wanne akiwemo Aslay, Mbosso, Beka Flavour na Enock Bella ambao walitenga anga na mawimbi ya tasnia ya burudani kwa miaka michache ambayo walikuwa pamoja.

Baada ya kutengana, waliokuwa na bahati kama Mbosso alipata nafasi ya kusajiliwa katika lebo kubwa nchini Tanzania, WCB Wasafi inayoongozwa na msanii nuli Diamond Platnumz, lakini pia wengine kama Aslay  na Beka Flavour walionekana wakifuata kila mmoja njia ya kwake binafsi katika safri ya muziki.

Wawili hao kwa miaka ya mwanzoni walifana na kazi zao kama wasanii wa kujitegemea kabla ya kuchimba mitini, lakini kwa mwenzao wa nne, Enock Bella, ilikuwa vigumu sana kujitambulisha yeye kama yeye na alisemekana kupotea mno kiasi kwamba wakati wenzake watatu wanazungumziwa, yeye hakuwepo kabisa katika picha.

Msanii huyo sasa ameibuka katika mahojiano ya kipekee aliyofanya na media ya Global TV Online nchini humo na kusema kuwa kuna kipindi Fulani alijaribu kujisogeza Wasafi ili kushikwa mkono lakini hilo halikufanikiwa.

Bella pia alisema kuwa anajiamini sana katika kipaji na kusema kuwa hata Mbosso kwenda Wasafi ilikuwa ni kupitia kipaji chake yeye.

“Naamini Wasafi waliamini talanta yangu na ndio maana waliweza kumchukua Mbosso. Kwa sababu msingemuona Mbosso kama sio talanta yangu pia,” Enock Bella alisema.

Msanii huyo alisema kuwa kipindi Mbosso yuko Wasafim naye alijaribu kuvizia kule ili kupata nafasi lakini licha ya kukaa nao kwa muda, hakuweza kuona mtu akimfikia na kusema kwamba acha huyu awekwe mahali, na hilo lilichangia mwenyewe kujiondoa tu na kuanza mihangaiko yake binafsi.

“Unachua mimi nimepitia sana changamoto nyingi, si tu kwenda Wasafi na ukaona hata nimeacha kuposti hata vitu vyao. Kuna maisha mengine pia na kuna watu wengine ambapo pia naamini ningekuwa nao karibu wangeweza kunisaidia. Mimi nilikuwa naona jitihada zangu ambazo nilikuwa nazifanya kwa Wasafi sana, lakini mbona kuna kitu nakikosa? Sawa nilikuwa naenda kwenye matamasha, lakini naplay part gani?”

“Nilipoona hili nilisema acha nijitenge na kama ninahitajka sana, nikiwa na umuhimu lazima nitaitwa tu kwamba Enock kaa hapa tufanye hivi. Kwa sababu nilishakaa sana karibu na uongozi ule lakini sikuweza kupata habari za muhimu kunihusu,” Enock alisema.