Wekeni bando tayari! Diamond na Nameless watangaza jambo lao kubwa Julai 14

Wasanii hao waliwataarifu mashabiki wao kujiweka tayari kwani Julai tarehe 14 itakuwa siku isiyo ya kawaida, watakuwa na jambo lao kubwa litakalouunganisha Afrika Mashariki yote.

Muhtasari

• Nameless ni mmoja wa wasanii wachache ambao walianza muziki wa Zaidi ya miongo miwili iliyopita na ambao hadi sasa bado wanazidi kutamba.

Diamond na Nameless watangaza jambo lao kubwa Julai 14.
Diamond na Nameless watangaza jambo lao kubwa Julai 14.
Image: Facebook

Kwa mara ya kwanza katika historia ya muziki wa Kenya na Tanzania, wasanii Nameless na Diamond wanatarajiwa kukutana kwenye tamasha ambalo litafanyika mwezi Julai nchini Uganda.

Tamasha hio ambalo limetangazwa kufanyika tarehe 14 Julai katika ukumbi maarufu wa Kololo litakuwa la kwanza kabisa kwa wababe hao wawili kukutana kwenye ukumbi mmoja.

Diamond kutoka Tanzania na Nameless kutoka Kenya ndio watakuwa wasanii wakubwa kutumbuiza kwenye tamasha hilo ambalo litakuwa linawajumuisha pia makumi ya wasanii wa Uganda.

Tamasha hilo litakuwa linaongozwa na mchekeshaji maarufu kutoka Uganda, Alex Muhangi na miongoni mwa wasanii wa Uganda ambao watapata nafasi adimu ya kutumbuiza na miamba hao wawili ni pamoja na King Saha, Spice Diana, Winnie Nwagi, Karole Kasita miongoni mwa wengine.

Nameless ni mmoja wa wasanii wachache ambao walianza muziki wa Zaidi ya miongo miwili iliyopita na ambao hadi sasa bado wanazidi kutamba na kupalilia jina lao katika tasnia ya Sanaa.

Vile vile, Diamond ni mmoja wa waanzilishi wa Sanaa ya kizazi kipya maarufu Bongo Flava nchini Tanzania na ambaye anakaribia miaka 15 kwenye gemu la Bongo.

Ikumbukwe siku mbili zilizopita, jukwaa la utiririshaji muziki la Boomplay lilimtangaza Diamond kuwa msanii wa kwanza kabisa kuwahi kutokea, ambaye amepiga namba na takwimu za juu Zaidi kwenye kukwaa hilo, kutoka ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Boomplay, Diamond almaarufu Simba ndiye msanii wa kwanza kupiga namba Zaidi ya milioni 300 kwenye takwimu za utiririshaji.