Arap Marindich ataja sababu ya kughairi kuchukua 'copyright' kwa meme yake

"Tuliona ilitusaidia kututangaza Zaidi kwa hiyo hatukuhisi hiyo athari yake hasi sana. Ilifanya hata akajulikana Zaidi,” - Meneja wake aliambia Radio Jambo.

Muhtasari

• “Kutokana na kusambaa kwa meme ile, makampuni nayo ikaingilia sasa hivi sisi ni balozi wa benki ya KCB,” alisema.

Arap Marindich, dereva aliyegeuzwa kichekesho kote duniani.
Arap Marindich, dereva aliyegeuzwa kichekesho kote duniani.
Image: Screengrab

Arap Marindich, dereva ambaye aligeuka kuwa meme mwaka jana kutokana na uwezo wake wa kuweza kukasirika na kutabasamu kwa wakati mmoja amevunja ukimya baada ya kutoweka kwenye rada ya watumizi wa mitandaoni kwa miezi kadhaa.

Picha za Marindich zilienea kote duniani, huku wakuza maudhui kutoka mataifa mbali mbali Afrika na Ulaya wakizituia kulinganisha matukio mawili ya kukinzana kwa wakati mmoja.

Mwanaume huyo kipindi hicho alipata umaarufu na hata katika mahojiano alidokeza kwamba alikuwa anatathmini kuchukua hakimiliki ya picha zake ili kufaidika kutokana na matumizi yake na watu mbalimbali mitandaoni kote duniani.

Katika mahojiano ya kipekee na mwandishi wa tovuti ya Radio Jambo, Marindich na Meneja wake waliweza kuzungumzia kuhusu mchakato wa kuchukua hakimiliki kwa picha hizo, lakini pia amekuwa akijishughulisha na nini baada ya kutozungumzia tena mitandaoni kwa wingi kama awali.

“Hatukuweza kuchukua hatua za kupata hakimiliki ya picha zile zilizotumiwa kama meme. Tuliona ilitusaidia kututangaza Zaidi kwa hiyo hatukuhisi hiyo athari yake hasi sana. Hatukuifuatilia kwa sababu kwa upande mwingine tuliona inatusaidia kutuuza sokoni Zaidi. Ilifanya hata akajulikana Zaidi maana watu walikuwa wanapakia huko Nigeria na makampuni nayo yakaingilia tukaina si vibaya,” Tula Chemoget, meneja wa Arap Marindich alisema.

Aidha, meneja huyo alifichua kwamba baada ya kupata umaarufu ule, alipata kuchukuliwa kama balozi kwa makampuni ya na hicho ndicho amekuwa akifanya kwa muda mrefu.

“Kutokana na kusambaa kwa meme ile, makampuni nayo ikaingilia sasa hivi sisi ni balozi wa benki ya KCB,” alisema.

Marindich alionekana mjini Naivasha wikendi iliyopita akipeperusha bendera ya benki ya KCB katika mashindano ya Safari Rally, ambapo pia alifichua kuwa yeye ni mpenzi mkubwa wa spoti hiyo.