Vinnie Baite atangaza nia ya kuweka rekodi ya Guiness kwa kutafuna Miraa '100 hours'

“Nitavunja Rekodi ya Dunia kwa kipindi kirefu zaidi cha Kutafuna Miraa. Masaa 100 ya kutafuna bila kuacha." - Baite.

Muhtasari

• Hata hivyo baadhi walipuzilia mbali changamoto hiyo kwa kile walisema kuwa Baite hali Miraa, kutokana mahojiano yake ya awali na podkasti ya Iko Nini.

Vinnie Baite ametangaza nia ya kuweka rekodi katika kutafuna Miraa.
GUINESS WORLD RECORD: Vinnie Baite ametangaza nia ya kuweka rekodi katika kutafuna Miraa.
Image: Facebook

Mchekeshaji ambaye aliwahi pia kuwa mtangazaji wa redio kwa kipindi Fulani nchini Vinnie Baite ametangaza kujitosa kwenye harakati za kuandikisha rekodi mpya ya Guiness World katika kula mirungi.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Baite aliandika ujumbe wa utani kwamba baada ya kutathmini kwa muda na pia kuona watu mbali mbali wakijitosa katika kuweka rekodi za Guiness World kwenye mambo mbalimbali, naye amepata wazo la kujikita katika utafunaji wa Miraa.

Baite alisema kwamba analenga kuweka rekodi hiyo kwa kuanza mchakato wa kutafuna Miraa kwa saa 100 mfululizo bila kukoma.

Mcheshi huyo aliwataka wafuasi wake kumpa msaada wa kumnunulia njugu na miraa pekee, kwani walaji wengi wa bidhaa hiyo hutumia njugu kama vitafunio.

“Nitavunja Rekodi ya Dunia kwa kipindi kirefu zaidi cha Kutafuna Miraa. Masaa 100 ya kutafuna bila kuacha. Ili kuunga mkono Jabathon yangu, tuma Miraa na njugu,” Baite aliandika.

Hata hivyo baadhi walipuzilia mbali changamoto hiyo kwa kile walisema kuwa Baite hali Miraa, kutokana mahojiano yake ya awali na podkasti ya Iko Nini.

Baite anatoka kaunti ya Meru ambapo upandaji wa miraa ndio kitega uchumi kikubwa.

Changamoto za kuweka rekodi za dunia zimekuwa zikifanywa na watu mbali mbali, ikiwa ni fursa ambayo iligunduliwa na mpishi wa Nigeria Hilda Baci aliyepika kwa Zaidi ya saa 100 mfululizo bila kukoma.

Baci baada ya kungoja kwa wiki kadhaa, hatimaye Guiness World Record walitambua juhudi zake na kumpa medali ya kuwa mshikilizi wa rekodi katika kitengo hicho cha kupika kwa muda mrefu.

Baadae pia mwanamke wa Kameruni alijitokeza akisema kuwa alikuwa amelenga kuweka katika kushiriki mapenzi kwa muda mrefu Zaidi, akilenga saa 200 mfululizo bila kukoma.

Mapema wiki hii, jamaa mwingine pia amejitokeza akisema kuwa alikuwa analenga kuandikisha rekodi ya dunia katika kipindi kirefu Zaidi cha kulia bila kukoma.

Kijana huyo alikuwa analenga kuweka rekodi ya saa 100.