2Mbili atangaza kujitosa mzima kwenye safari ya kuweka rekodi mpya ya Guiness dunia

Rekodi ya Guiness ya dunia imekuwa kama kivutio kwa watu wengi Afrika huku sasa ikiwa kama fasheni ambayo kila mmoja anajaribu kufikiria cha kufanya ili kuandikisha rekodi mpya.

Muhtasari

• "...kuanzia Ijumaa hii, kwa hiyo nawaomba mkuje mniunge mkono kwa hiyo kuwa tayari,” 2Mbili alisema.

• 2mbili ambaye aliwasuta watu kwa kula chakula katika shindano la mpishi  Maliha aliyelenga kuweka rekodi ya kupika ndani kwa muda mrefu aliwataka watu kujitokeza ili kumsapoti.

2Mbili
2Mbili
Image: Instagram

Mchekeshaji na mkuza maudhui wa YouTube 2Mbili ametangaza rasmi kwamba Ijumaa alianza safari ya kuweka rekodi mpya ya Guiness duniani katika kulala.

Akizungumza na SPM Buzz, 2Mbili alisema kwamba anatarajia kuweka rekodi mpya ya dunia katika kulala kwa muda mrefu Zaidi bila kuamka, na kuwaomba watu kujitokeza kumuunga mkono anapolenga kufanikisha hio.

“Nataka kuwaambia kwamba nitajaribu kuvunja rekodi kusema kweli, ya kulala kwa muda mrefu Zaidi kuanzia Ijumaa hii, kwa hiyo nawaomba mkuje mniunge mkono kwa hiyo kuwa tayari,” 2Mbili alisema.

Mchekeshaji huyo alisema haya ikiwa ni siku chache baada ya kuwasuta watu maarufu nchini kwamba walikwenda katika hafla ya mpishi wa Kenya aliyelenga kuvunja rekodi ya dunia na badala yake kula vyakula vyote.

Mpishi Maliha alianzisha mchakato wa kuweka rekodi ya kupika ndani ya nyumba kwa muda mrefu Zaidi wikendi iliyopita ambapo alipika kwa Zaidi ya saa 80 lakini 2Mbili aliibua madai kwamba watu maarufu waliojitokeza kama njia moja ya kumuunga mkono wengi wao walikula chakula hicho ambacho mpishi huyo alikuwa amenuiwa kukitoa kama msaada kwa watu wasio na chakula haswa wale wa kuzurura mitaani.

"Hongera mpishi Maliha, Kwa bahati mbaya hakutakuwa na kitu cha kuchangia watoto wa mitaani kama ilivyopangwa mapema kwa sababu watu mashuhuri walikuja na kula chakula chote (kwa maudhui)" Aliandika kwenye hadithi zake za Instagram.

Wengine walibeba hadi nyumbani kwao kwa jina la tumekuja kuku support” 2mbili aliongeza.

Bila kutaja majina pia aliwaita baadhi wasanii kwa kubadilisha mazingira ya shindano hilo kuwa kiungo cha burudani.