DJ Pierra Makena afichua maswali magumu anayoulizwa na bintiye kuhusu babake

"Maswali ambayo anauliza ni ‘lakini niliwahi kumuona, wa hiyo ako wapi?’ lakini wakati anauliza huwa namjibu unajua ‘babako alisafiri’ au ‘ako tu bize atakuja mkutane ako mbali kikazi’…" alisema.

Muhtasari

• “Naamini wakati atakuwa mtu mzima, atajua dunia ikoje, na natumai hatokuja kulifikiria kwa njia hasi.”

DJ Pierra Makena.
DJ Pierra Makena.
Image: Instagram

DJ Pierra Makena amefunguka kwamba kumlea mtoto bila uwepo wa baba katika maisha yake kunakuja na changamoto si haba.

Akizungumza katika mahojiano na Mungai Eve, Makena alifichua kuwa binti yake wa miaka 7 ambaye hajawahi muonesha baba yake tangu kuzaliwa.

Alisema kwamba baba mwanawe alimtoroka akiwa na mimba ya wiki mbili na kufunga ndoa miezi mitano baadae na hiyo ndio mara ya mwisho walionana na yeye wakiwa katika mahusiano.

Makena alisema kwamba haijakuwa rahisi kumlea binti kwa miaka 7 pasi na kuwepo kwa baba na akasema kwamba mtoto huyo humkabili na maswali magumu sana.

Makena alifichua kwamba wakati mwingine mtoto anamuuliza baba yuko wapi na inambidi kuibua majibu ya kughushi ilmradi tu kumtuliza.

“Wakati anauliza maswali kama hayo kuhusu babake, ana wazo kwa mbali kuhusu babake lakini maswali ambayo anauliza ni ‘lakini niliwahi kumuona, wa hiyo ako wapi?’ lakini wakati anauliza huwa namjibu unajua ‘babako alisafiri’ au ‘ako tu bize atakuja mkutane ako mbali kikazi’… huwa najaribu kukwepa masuala kama hayo lakini pia huwa najaribu kumhakikishia kwamba ‘unajua babako anakupenda’ ili tu kuhakikisha kwamba haimuathiri kwa njia hasi,” alisema.

Makena alisema kwamba huwa inamlazimu kumdanganya mtoto kwamba babake anampenda japo kuwa wakati mwingine si kweli lakini ni kwa ajili tu ya kumhakikishia mtoto upendo kutoka kwa mdomo wake.

Lakini pia alisema kwamba hatolificha hilo kwa muda wote kwani mtoto atakua na atajua jinsi dunia ilivyo na kujua kutenganisha maji na mafuta.

“Naamini wakati atakuwa mtu mzima, atajua dunia ikoje, na natumai hatokuja kulifikiria kwa njia hasi.”