'Usikuje mkono mtupu!' Akothee akaribisha mashabiki kusherehekea digrii baada ya miaka 14

" Ninatarajia uwepo wako na msaada. Kanuni ya mavazi. Suti nyeusi. Usikuje na mkono tupu Haki 🤣🤣🤣🤣” alimaliza kwa emoji za kucheka.

Muhtasari

• Akothee alisema kwamba siku hiyo itakuwa ya kusherehekea kufuzu kwake kwa kupata digrii ambayo aliifukuzia kwa miaka 14.

Akothee
Akothee
Image: Facebook

Msanii na mjasiriamali Esther Akoth Kokeyo, maarufu kama Akothee amethibitisha kwamba Desemba 10 itakuwa siku yake kuu ambapo ataandaa tafrija ya ndovu kumla mwanawe katika eneo la Rongo, kaunti ya Migori.

Akothee kupitia ukurasa wake wa Facebook alichapisha mabango ya kutoa mialiko kwa mashabiki wake wote ambao wamekuwa wakimuamini katika kile ambacho amekuwa akikifanya si tu katika muziki bali pia katika kuinua jamii.

Akothee alisema kwamba siku hiyo itakuwa ya kusherehekea kufuzu kwake kwa kupata digrii ambayo aliifukuzia kwa miaka 14.

Alisema kwamba alilazimika kuweka kwenye akiba mara kadhaa ndoto yake ya kupata digrii kwa miaka hiyo yote ili kuiendeleza jamii yake lakini hatimaye amefanikiwa kumaliza.

“Mashabiki wapendwa, Umealikwa kwa moyo mkunjufu kuungana nami katika kusherehekea safari ya ajabu mnamo tarehe 10 Desemba 2023 katika Chuo cha Akothee huko Rakwaro, eneo bunge la RONGO, kaunti ya Migori. Baada ya miaka 14 ya kusitisha elimu yangu ili kuwawezesha wengine, ninajivunia kutangaza kukamilika kwa shahada yangu katika Chuo Kikuu cha Mt Kenya,” Akothee aliandika.

Alisema pia kwamba siku hiyo itakuwa ya kuzindua rasmi shule yake ya Akothee Foundation Academy ila akasisitiza kwamba mashabiki wanaotarajia kujitokeza katika shughuli yake wasiende mikono mitupu.

Kuhusu mavazi ya siku hiyo, Akothee alisema si vibaya kwa watu kuvalia suti nyeusi.

“Kwa pamoja, tukumbuke mafanikio haya na kuanzishwa kwa Akothee Academy, tukisisitiza umuhimu wa elimu. Ninatarajia uwepo wako na msaada. Kanuni ya mavazi. Suti nyeusi. Usikuje na mkono tupu Haki 🤣🤣🤣🤣” alimaliza kwa emoji za kucheka.