Pasta Ng'ang'a afichua sababu ya kununua simu ya Sh240k ambayo hapendi kutumia (video)

"Unajua mimi hata situmii simu. Mimi ni WhatsApp na Facebook na YouTube, hizo zingine huwa situmii." Ng'ang'a alifichua.

Muhtasari

• Mchungaji huyo aliwasuta wale wanaotumia pesa nyingi kununua simu na kusema kwamba hakuna haja ya kununua simu ghali kwa mkopo kama huna pesa.

Pasta Ng'ang'a
Pasta Ng'ang'a
Image: Screengrab

Mchungaji James Ng’ang’a wa kanisa la Neno Evangelism amewashangaza waumini wake baada ya kuwatajia kiasi kikubwa cha fedha alizotumia kununua simu yake ya rununu ambayo hata hivyo hapendi kuitumia sana.

Ng’ang’a ambaye anajulikana kwa mahubiri yake ya ucheshi na ya kujitapa alikuwa anahubiri katika ibada ya kanisa lake kwenye klipu moja ambayo imewavutia wengi mitandaoni.

Mchungaji huyo aliwasuta wale wanaotumia pesa nyingi kununua simu na kusema kwamba hakuna haja ya kununua simu ghali kwa mkopo kama huna pesa.

“Utaendaje kununua simu ya elfu 20 ukopeshwe na Safaricom uwe unalipa kila siku? Labda tu kama wewe ni mjinga. Simu ya elfu 20! Ukitembea itabidi tu akili zako ziwe kwa hiyo simu,” Ng’ang’a alihubiri.

Ghafla alijongea karibu na kiti chake kwenye madhabahu na kurudi na simu yake mkononi.

Cha kushangaza, katika mahubiri yake kuhusu simu za bei rahisi, Ng’ang’a aliwaambia waumini wake kuwa simu yake aliinunua kiasi cha shilingi laki mbili na 40 elfu.

Mchungaji huyo alisema kwamba alipatiwa zawadi ya shilingi elfu 160 kununua simu naye akajiongeza na kufikisha elfu 240 lakini akadai kwamba simu hiyo hapendi kuitumia sana.

Ng’ang’a alisema kwamba simu yake kazi kuu moja inafanya ni kuonesha haiba yake akiwa miongoni mwa wachungaji wengine katika mikutano ya haiba ya juu.

“Hii yangu ni ya 240k, Nilipewa na mtu 160k ninunue simu, basi nikaongeza. Sasa hii simu pasta, unataka kununua hii simu ya nini? Unajua mimi hata situmii simu. Mimi ni WhatsApp na Facebook na YouTube, hizo zingine huwa situmii. Lakini kwa sababu ya hadhi yangu, tukienda pale [mikutanoni] naweka hapo kwa meza…” Ng’ang’a alisema.

Licha ya kuwa na mahubiri ya kuchekesha akionekana kama anawagombanisha au kuwadunisha waumini wa kanisa lake, kila wiki kanisa la mchungaji huyo hufurika na watu wanaokwenda kwa ajili ya maombi ya mujiza.

Ng’ang’a aligonga vichwa vya habari wiki chache nyuma baada ya klipu kuvuja akimdhihaki muumini mmoja aliyetoa dhabiu ya shilingi 500 kwa ajili ya maombi maalum.

Katika klipu hiyo, Ng;ang’a alionekana akikataa kufanya maombi kwa shilingi 500, akisema kwamba kiasi hicho cha pesa hakiwezi kikafanya chochote cha mno katika uchumi wa sasa uliozorota.